2017-04-02 14:18:00

Ziara ya Papa Francisko Jimboni Carpi, Italia


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya V ya Kipindi cha Kwaresima, tarehe 2 Aprili 2017 ametembelea Jimbo Katoliki la Carpi, Italia ili kuonesha mshikamano wake wa pekee kwa familia ya Mungu eneo la Emiglia Romagna lililoathiriwa na tetemeko la ardhi miaka mitano iliyopita. Jimboni humo amepata nafasi kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Mashuhuda, akabariki mawe ya msingi kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Agatha, Nyumba ya Mafungo ya kiroho ya Sant’Antonio in Novi pamoja na majengo ya Shirika la huduma la Kanisa Katoliki, Caritas, Carpi.

Baba Mtakatifu Francisko amepata chakula cha mchana na Wakleri, Mapadre wazee na waseminari wa Jimbo Katoliki la Carpi. Baadaye majira ya alasiri amekutana na kuzungumza na: wakleri, watawa na majandokasisi kwenye Kikanisa cha Seminari ya Jimbo la Carpi, baadaye ametembelea Kanisa kuu la Mirandola na kuzungumza pamoja na watu walioathirika kwa tetemeko la ardhi kunako mwaka 2012 na kusababisha watu 27 kupoteza maisha pamoja na uharibifu mkubwa wa makazi ya watu na miundo mbinu katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa iliyoadhimishwa kwenye Uwanja wa Mashuhuda amekazia kwa namna ya pekee kuhusu: ukuu wa Mungu anayejifunua kuwa chechemi ya maisha dhidi ya kifo, ushuhuda uliotolewa na Kristo Yesu kwa kumfufua Lazaro siku chache kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake. Yesu aliguswa na maombolezo na kilio cha ndugu na jamaa zake Lazaro ambao walidhani kwamba, kwa kifo cha Lazaro, yote yalikuwa yamekwisha! 

Mwenyezi Mungu anaonesha kuwa mbali na dhambi, lakini daima yuko karibu na wale waliopondeka moyo, watu wanaoteseka; akayapatia mateso kisogo kwa kuyaambata mwenyewe, kama alivyofanya Yesu kwa kumlilia Lazaro mfu! Yesu anachukua fursa hii kuwaimarisha ndugu zake Lazaro katika imani na matumaini ya ufufuko kwa kuenda kaburini na kwa njia ya sala yake. Katika Fumbo la mateso na mahangaiko ya binadamu anasema Baba Mtakatifu, Kristo Yesu anatoa mfano bora wa kuigwa, kwani hayakimbii mateso ambayo kimsingi ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na kamwe hakubali mateso haya kumfungia ndani mwake! Mbele ya kaburi la Lazaro kuna kinzani na hali ya kukata tamaa kutokana na simanzi ya kifo cha Lazaro, hali inayoonesha hata giza la maisha ya ndani. Lakini, waamini wanakumbushwa kwamba, wameumbwa ili kuishi, mateso na mahangaiko yanaonesha kiu ya maisha ya uzima wa milele dhidi ya kifo na mauti. Yesu ni shuhuda wa matumaini dhidi ya kifo, ubaya na dhambi kwa kutangaza na hatimaye kwa wakati muafaka kushuhudia Ufufuko na maisha mapya, kwani anasema kila aishiye na kumwamini hatakufa kabisa milele bali ataishi, ndiyo maana akamfufua Lazaro kutoka kaburini.

Baba Mtakatifu anawaambia waamini wanaweza kuchagua kusimamia upande gani! Yaani upande wa kaburi kwa kumezwa na simanzi pamoja na kifo au upande wa Yesu kwa kuwa na matumaini ya ufufuko wa wafu, kwani kwa njia msaada wa Mungu anaweza kuwainua wale wanaogalagala udongoni na kuanza mchakato wa ujenzi wa matumaini yenye uvumilivu na kwamba, katika shida na mahangaiko ya binadamu; Yesu daima anapenda kuonesha ukaribu wake.

Baba Mtakatifu anaikumbusha familia ya Mungu Carpi kwamba, hata wao, kila mmoja wao analo kaburi lake, madonda, huzuni na majonzi pamoja na dhambi ambayo bado inaendelea kumtesa. Haya ni maeneo ambayo wanapaswa kuyatambua ili kumwalika Yesu aweze kuyatembelea na hatimaye, kuwapatia faraja na pumziko! Mwenyezi Mungu anataka kukutana nao katika Njia ya Maisha, Imani na Ufufuko katika roho badala kuendelea kulalama katika hofu, ubaya na dhambi. Yesu anapenda kuwaalika kutoka katika mazingira ambayo hayana tena matumaini; mazingira yanayosongwa songwa kwa hofu na udhaifu wa binadamu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, daima matatizo na magumu yatamwandama mwanadamu, lakini kwa kumfuasa Kristo Yesu watakirimiwa uthabiti wa maisha kwani Yesu ni ufufuo na maisha; ni chemchemi ya furaha na faraja ya moyo; matumaini yanayochipua; mateso na mahangaiko yanayogeuzwa kuwa ni amani; fadhaa inageuka kuwa imani na majaribu yanayotolewa kuwa ni sadaka ya upendo. Yesu daima ataendelea kutembea na waja wake kwa kuwashika mkono ili kuwategemeza, kwa kuwatia shime kwa Neno lake ili waweze kumwendea na kutembea kwa pamoja.

Leo, Yesu anawaalika waamini kuondoa jiwe katika historia ya maisha yao ya dhambi na aibu yake ili Yesu aweze kuingia ndani mwao. Huu ni muda uliokubalika wa kutubu na kumwongokea Mungu;  kwa kuachana na malimwengu mambo yanayowakwamisha. Kwa kutembelewa na kuokolewa na Yesu, waamini wawe na ujasiri wa kuomba neema ya ushuhuda wa maisha kwa walimwengu mamboleo ambao kimsingi wana kiu ya mashuhuda wenye mvuto na mashiko; wanaohamasisha na kuchochea matumaini na furaha ya Kristo Mfufuka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.