2017-04-01 14:13:00

Utu na heshima ya binadamu ni kipimo msingi cha maendeleo ya kweli!


Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, kuanzia tarehe 3 – 4 Aprili, 2017 Baraza lake litaadhimisha Mkutano wa Kimataifa kuhusu Miaka 50 tangu Waraka wa Kitume wa Mwenyeheri Paulo VI “Populorum progressio” yaani “Maendeleo ya watu” ulipochapishwa rasmi. Lengo la mkutano huu ni kufanya upembuzi yakinifu kuhusu misingi ya kitaalimungu, kiutu na kichungaji inayofumbatwa katika Waraka huu mintarafu uhusiano wake na wale wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika ustawi na maendeleo ya binadamu.

Mwenyeheri Paulo VI miaka 50 iliyopita alichapisha Waraka wa Kitume: “Populorum progressio” yaani “Maendeleo ya watu” akiwataka watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kushikamana kwa dhati katika kukuza na kudumisha amani kwani hili ni jina jipya la maendeleo endelevu ya binadamu! Ni Waraka unaowahimiza watu wote kujizatiti katika kulinda na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu kwa kushirikiana na kushikamana katika upendo wa kidugu! Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walisema uchungu na fadhaa ya mwanadamu wa nyakati hizi hasa maskini na wanaoteseka ni uchungu na fadhaa ya Kanisa pia. Mwenyeheri Paulo VI alipenda kumwilisha changamoto zilizokuwa zimeibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu: maisha na changamoto za Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Kardinali Turkson anasema mchango wa Kanisa katika mchakato wa maendeleo endelevu sehemu mbali mbali za dunia ni mkubwa na unashuhudiwa na wengi hususan katika elimu, afya na maendeleo endelevu ya binadamu. Hii ni asili na utume wa Kanisa katika dhamana ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili ili kulinda utu na heshima yake, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Baraza la Kipapa la huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu linataka kuzivalia njuga changamoto za maendeleo endelevu ya binadamu ili kuzipatia majibu muafaka kwa njia ya mwanga wa Injili.

Hii ni changamoto ya kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, utu na heshima ya binadamu; uhuru wa kuabudu na kwamba, sera na mikakati ya uchumi na maendeleo inapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi na wala si rasilimali fedha na vitu! Watu wajengewe uwezo wa kiuchumi ili kupambana vyema na mazingira na hatimaye, yaweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi! Kardinali Turkson anahitimisha mahojiano maalum na Radio Vatican kwa kusema, Kanisa litaendelea kujadiliana na kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ili kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata huduma ya elimu makini na afya bora vigezo muhimu sana katika kuchochea ustawi na maendeleo endelevu ya watu! Itakumbukwa kwamba, chimbuko la Umoja wa Mataifa ni mafao, ustawi na maendeleo ya watu! Utu na heshima ya binadamu inapaswa kuwa ni kigezo muhimu sana cha kukuza na kudumisha uchumi shiriki na endelevu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.