2017-04-01 10:45:00

Papa Francisko: Ijumaa ya huruma ya Mungu: Matendo ya huruma!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ilikuwa ni nafasi ya pekee kwa waamini kutambua na kuonja ndani mwao huruma na upendo wa Mungu ambao kimsingi ni kazi ya Mungu na mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu. Mwenyezi Mungu anahangaika na anapenda kuwaona watoto wake anasema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume,  “Misericordiae vultus” yaani Uso wa huruma, wakiwa na afya njema, furaha na amani tele! Huu ndio upendo na huruma ambayo waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuimilisha katika uhalisia wa maisha, kwa kupenda na kuhurumia kama Mungu anavyopenda na kuwahurumia watoto wake.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 31 Machi 2017 amerudia tena utaratibu aliokuwa amejiwekea wakati wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kuadhimisha Ijumaa ya huruma ya Mungu; siku ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwa kutembelea Kituo Kikuu cha Vipofu na Viziwi cha Mkoa cha S. Alessio – Margherita wa Savoia kilichoko mjini Roma. Kituo hiki pia kiliwahi kujulikana kama “Cristoforo Colombo”, kinachojihusisha kwa karibu sana kuwahudumia watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na ulemavu wao. Kuna baadhi ya watu wamezaliwa na ulemavu huo na wengine wamepata kilema hiki kutokana na magonjwa mbali mbali. Kuna watoto 50 wanaopata elimu maalum kwa ajili ya kuwasaidia kuendesha maisha yao ya kila siku na watu wazima 37 wanaopata huduma Kituoni hapo. Baba Mtakatifu amepata fursa ya kuzungumza na kusalimiana na walemavu hawa na mwishoni akawaachia zawadi ya picha iliyotiwa mkwaju wake kama kumbu kumbu ya kutembelea kituo ni hapo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.