2017-04-01 13:46:00

Madhabahu ya Kanisa ni vituo muhimu vya Uinjilishaji Mpya!


Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya kuanzia sasa limepewa dhamana na madaraka ya kusimamia Madhabahu ya Kimataifa kadiri ya sheria za Kanisa; Kuhakikisha kwamba, maeneo haya muhimu katika maisha na utume wa Kanisa yanakuwa ni mahali pa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kusaidia madhabahu ya Kanisa kuwa ni mahali pa mikutano ya kitaifa na kimataifa, ili kukuza na kudumisha ibada za watu na hija kwenye maeneo matakatifu. Baraza litakuwa na dhamana ya kuwafunda wahudumu kwenye madhabahu haya ili yaweze kutoa huduma msingi za kichungaji, kikanisa na maisha ya kiroho pamoja na kuendeleza sanaa na utamaduni wa maeneo haya kama mifumo maalum ya uinjilishaji.

Kimsingi haya ndiyo yaliyomo kwenye barua binafsi iliyoandikwa na Baba Mtakatifu Francisko ijulikanayo kama “Sanctuarium in Ecclesia”  yaani “Madhabahu ndani ya Kanisa” iliyozinduliwa rasmi 1 Aprili 2017. Baba Mtakatifu anasema, madhabahu yana umuhimu wa pekee kabisa katika maisha na utume wa Kanisa. Hapa ni mahali pa hija na ungamo la imani, ni chemchemi ya imani na matumaini yanayobubujika kutoka katika undani wa mtu! Ni kielelezo cha umissionari wa watu wa Mungu, mahali pa sala, tafakari ya Neno la Mungu na kujiaminisha katika huruma na upendo wa Mungu. Tangu mwanzo madhabahu yamekuwa ni mahali pa kwenda kutafakari kuhusu Fumbo la Umwilisho, Fumbo la Pasaka kiasi cha kuibua ibada kwa Bikira Maria, Mitume, Watakatifu na Wenyeheri.

Baba Mtakatifu anaendelea kukaza akisema, madhabahu ni mahali ambapo waamini wanashuhudia imani yao na kuonja uwepo wa daima wa Mwenyezi Mungu katika maisha yao; Uwepo wa Bikira Maria na Watakatifu wanaowaonjesha huruma na upendo kazi kubwa ya Roho Mtakatifu. Madhabahu yameunda na kujenga utamaduni wa baadhi ya familia na mataifa. Kumekuwepo na makundi makubwa ya mahujaji, yanayotaka kusali, kuadhimisha Liturujia ya Kanisa na kumshukuru Mungu kwa neema na baraka zake katika safari ya maisha yao. Kimsingi madhabahu ni mahali pa uinjilishaji mpya!

Baba Mtakatifu anasema, licha ya watu kukengeuka na kutopea katika imani, waamini wengi wamegundua kwamba, madhabahu ni mahali pa kujipumzisha na kujichotea nguvu katika hali ya ukimya na tafakari nje kabisa ya purukushaji za maisha ya kila siku! Hapa waamini wanaonesha ile kiu ya kutaka kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, kwa kugundua undani wa maisha yao, kutubu na hatimaye kumwongokea Mungu. Licha ya huduma za kichungaji zinazotolewa Parokiani, lakini madhabahu pia ni chemchemi ya msaada wa kichungaji na uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wa maisha.

Madhabahu ni mahali pa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu; mahali muafaka pa kuadhimisha Sakramenti za Kanisa hasa: Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu; mahali pa ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Hapa ni mahali ambapo mwamini anafundwa namna ya kuinjilisha, kwa kuwajibika katika majiundo makini ya Kikristo yanayoshuhudiwa katika matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji. Ni kituo muhimu sana cha Katekesi kwa Jumuiya ya Kikristo ili kuimarisha imani, matumaini na mapendo. Madhabahu ni chemchemi ya faraja kwa wagonjwa, walemavu, maskini, wakimbizi na wahamiaji pamoja na wale wote wanaosukukizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko kwa kuangalia dhamana hii kubwa, ameamua kuhamishia madaraka na dhamana ya kusimamia shughuli za madhabahu ya kimataifa chini ya usimamizi wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya; dhamana ambayo hapo awali ilikuwa inatekelezwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.