2017-03-31 14:58:00

Juhudi zifanyikeTanzania kutokomeza ukatili dhidi ya walemavu wa ngozi!


Mkutano ulioshirikisha wadau wa haki za binadamu umefanyika Alhamisi Dar es Salaam kuhusiana na haki za watanzania wenye ulemavu wa ngozi (Albino) ambapo kwa sasa kuna tuhuma za ufukuaji wa makaburi yao. Mkutano wa tume ya haki za binadamu na utawala bora jijini Dar es Salaam umewashirikisha wadau kutoka mahakama, taasisi za kiraia, ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali , na tume ya kurekebisha sheria.
Washiriki wote ni wadau muhimu katika mapambano ya kutafuta haki za watu wenye ulemavu wa ngozi, na mmbapo taarifa inasema kwamba wakati juhudi hizi zinafanyika kumekuwa na ripoti kuwa watu wenye ulemavu wa ngozi makaburi yao sasa yanafukuliwa licha kuwepo mauaji, utekaji, na ukataji wa viungo vyao.Mwenyekiti wa tume ya haki za binadamu na utawala bora Bahame Nyanduga amesema kuwa tathmini iliyofanywa na tume inaonyesha kuwa tatizo hili limekuwepo tangu mwaka 2006, lakini linaonekana hivi sasa limejitokeza kwa nguvu.

Amesema "Napenda kuwashukuru kwa kuliibua tatizo hili kwani inaonekana watu hawa walinyimwa haki zao wakiwa hai na sasa wananyimwa haki zao hali ya kuwa wameshakufa”.Aidha amezitaka Wizara ya Serikali za Mitaa chini ya ofisi ya Rais pamoja na halmashauri zake watizame jinsi ya kutenga mafungu katika bajeti kwa ajili ya kutoa elimu itakayo ondoa unyanyapaaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi na kutokomeza ukatili wanaofanyiwa. Kwa upande wa wadau  wa haki za binadamu walitaka kuwepo sheria kali zaidi kwa watakaokutwa na hatia katika kesi zinazohusisha watu wenye ulemavu wa ngozi. Wametaka kuwa elimu ya haki za binadamu ianze kutolewa kuanzia ngazi za chini.

Naye mwakilishi wa shirika la kimataifa la utetezi wa watu wenye ulemavu wa ngozi la (under the same sun), Vicky Mtetema ameomba kuwepo na takwimu sahihi za matukio yanayohusiana na ukatili wa watu wenye ulemavu wa ngozi ikiwemo matukio ya hivi karibuni ya ufukuaji wa makaburi waliozikwa.Ripoti inasema kuwa tangu kuanza kwa ukatili huu dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini imeelezwa kwamba jumla ya kesi 65 za watuhumiwa wa mauaji na ukatili wa watu hao zimefikishwa kwenye vyombo mbalimbali vya Mahakama huku kesi saba zikiwa zimetolewa hukumu.

Na Dina Chahali

Wakilishi wa Idhaa ya Kiswahili Voa,aliyeko Tanzania

 








All the contents on this site are copyrighted ©.