2017-03-31 14:13:00

Bwana Kofi Annan kutoa wito wa mapambano dhidi ya Tabianchi


Katibu mkuu wa zamani wa umoja wa Mataifa Kofi Annan,mapema wiki hii  ametoa wito kwa dunia kuendelea na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi licha ya uamuzi wa rais wa Marekani Donald Trump kutoa amri ya kuondolewa kwa sheria zilizokuwa zimetiwa saini na mtangulizi wake Barack Obama kuhusu taifa hilo kuwa na nishati salama. Annan amesema haya wakati akihutubia kwenye mkutano wa mwaka wa mfuko wake kuhusu kilimo jijini Brussels, ambapo amesisitiza kuwa makubaliano yaliyotiwa saini jijini Paris yaliweka nia nzuri ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Bwana Kofi Annan anasema Marekani inaweza kujitoa kwenye makubaliano hayo kutokana na sera za raisa Trump au ikaamua kusitisha kwa muda utekelezaji wake, lakini dunia haipaswi kusimama kwa sababu Marekani imeamua kufanya yote haya.Mshindi huyu wa zamani wa tuzo ya Nobel, amegusia pia kuhusu madhara ya mabadiliko ya tabia nchi na namna gani nchi zinaweza kuboresha mfumo wa chakula ili kulisha mamilioni ya watu duniani wanaokabiliwa na baa la njaa kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kofi Annan ameeleza umuhimu na mahitaji ya uwekezaji wa nguvu kwenye nchi zinazoendelea na mfumo wa chakula ambao utawezesha kuzalisha chakula kwa wingi kwa kutumia rasilimali chache.Katibu mkuu huyo wa zamani ametoa wito kwa nchi duniani kuhakikisha zinawajibika na kutoa mchango wao katika kuhakikisha zinatekeleza na kufikia maendeleo endelevu kama yalivyoainishwa kwenye mkataba wa umoja wa Mataifa.
Matamshi ya Annan yamekuja ikiwa ni saa chache tu zimepita toka rais wa Marekani, Donald Trump atie saini amri ya kuondoa mikataba iliyokuwa imewekwa na mtangulizi wake kwenye matumizi ya nishati ya makaa ya mawe, akisema sheria zilizokuwa zimewekwa zinawanyima raia wa Marekani ajira.Wataalamu wa masuala ya mazingira wanaonya kuwa uamuzi wa rais Trump hautakuwa na madhara tu ndani ya Marekani lakini pia utakuwa na madhara kidunia.likadhalika kuhusu suala la  wahamaiaji, Bwana Annan anasema matukio haya ni ya kihistoria lakini inabidi kutafua mbinu za kutekeleza na hasa zinazohusu asili ya wahamiaji, mahala wanapotoka na mahala wanapotazamia. Hiyo ni kwasababu amesema iwapo sera za nchi wanazotoka, zinatoa ari na ambayo inawezesha kuishi kiutu,hiyo inaweza kusaidia kupunguza hali ya kuhamahama.

Ikumbukwe hata mwezi Januari  Christine Todd Whitman ,ambaye ndio mkuu wa shirika la kulinda mazingira nchini Marekani alikuwa amemshtumu Donad Trump kwa kupuuza ripoti za sayansi.Na alionya kwamba tishio lake la kuondoa sera za kulinda hali ya anga linaweka siku za usoni hatarini , na wakati huo huo wafuasi wa Trump walikuwa wanasema  kuwa sheria za hali ya anga na kawi zinaharabu biashara. Hata hivyo  Bi Todd Whitman alikuwa amejibu kuwa Marekani inapaswa kutafuta njia za kukuza biashara bila kuharibu mazingira.

Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.