2017-03-30 11:30:00

Vijana ni mashuhuda wa furaha ya Injili!


Kanisa linapenda kuwasindikiza vijana katika maisha na utume wao, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili katika medani mbali mbali za maisha. Kanisa litaendelea kujenga  na kuimarisha utamaduni wa kuwasikiliza na kutembea na vijana wa kizazi kipya ili kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi magumu katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua umuhimu wa utume wa vijana, ameamua kuitisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa kunako mwezi Oktoba, 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito”.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa ni wadau wakuu katika maadhimisho haya na kwamba, Kanisa liendelee kutafakari changamoto zinazowasibu vijana wa kizazi kipya ili kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi! Ni katika mantiki hii, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, CCEE, kuanzia tarehe 28 – 31 Machi 2017 linaadhimisha Kongamano la Vijana Barani Ulaya linaloongozwa na kauli mbiu “Kuwasindikiza Vijana ili kujibu kwa uhuru kamili wito wa Kristo”. Jimbo kuu la Barcellona ndilo mwenyeji wa Kongamano hili kwa mwaka 2017.

Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya amesisitiza kwa namna ya pekee umuhimu wa vijana kusimika maisha na vipaumbele vyao katika tunu msingi za maisha ya Kikristo, tayari kushiriki katika ujenzi wa familia kubwa ya binadamu, mahali ambapo: utu, heshima na utakatifu wa maisha vinathaminiwa na kupewa kipaumbele cha pekee. Vijana Barani Ulaya wanapaswa kufanya upembuzi yakinifu ili kuangalia kwa makini changamoto zinazowasibu kwa wakati huu ili kujiwekea mikakati kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, ikiwa kama kweli Bara la Ulaya linataka kuendelea kuonesha ile sura ya ujana!

Itakumbukwa kwamba, hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anazungumza na wakuu wa Umoja wa Ulaya kama sehemu ya maadhimisho ya Miaka 60 ya Mkataba wa Roma. Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Barani Ulaya kwa kiasi kikubwa anasema Kardinali Angelo Bagnasco yanasimikwa katika umoja na mshikamano; kwa kuwekeza katika elimu makini kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuwapatia fursa za ajira ili kuweza kutekeleza ndoto za maisha yao. Vijana wanapaswa kuwa na imani na Umoja wa Ulaya, ili waweze kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utakatifu wa maisha yabinadamu; uhuru wa kweli na uwajibikaji unaotekelezwa na kila mtu kadiri ya dhamana na nafasi yake katika jamii. Vijana wanahamasishwa kumwilisha ndani mwao mshikamano unaofumbatwa katika kanuni auni; maadili na utu wema kwa kukataa kishawishi kinachotaka kuwadhalilisha binadamu wengine!

Kardinali Vincent Nichols, Makamu wa Rais, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya katika mahubiri yake kwenye misa ya ufunguzi wa kongamano la Vijana Barani Ulaya, amekazia umuhimu wa vijana kumkimbilia na kumwambata Kristo Yesu ili aweze kuzima kiu ya maisha na matumaini ya ujana wao. Vijana wawe kweli ni mashuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, changamoto na mwaliko wa kuendelea kushiriki maisha ya uzima wa milele kwa njia ya Sakramenti za Kanisa na kwa namna ya pekee: Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho.

Vijana waendelee kumtumainia Roho Mtakatifu anayelisimamia na kulitegemeza Kanisa; Roho Mtakatifu anayelitakasa Kanisa na kuwaponya waamini wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao; Roho Mtakatifu anayewawezesha waamini kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu kama ushuhuda wa imani tendaji.  Roho Mtakatifu ndiye anayewapatia waamini jeuri ya kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Kongamano la Vijana Barani Ulaya linapania kuwasaidia vijana kung’amua mapenzi ya Mungu katika maisha yao, daima wakipania mambo makuu!

Yote haya anasema Kardinali Nichols yanapatikana kwa kujinyenyekesha kwa Roho Mtakatifu ili kumwachia nafasi ya kuwapatia hamasa katika maisha, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Vijana wamepokea zawadi ya Roho Mtakatifu katika maisha yao, kumbe, hata wao wanapaswa kuwa ni zawadi inayopendeza kwa Mungu na jirani zao, tayari kushiriki katika mchakato wa kazi za Ukombozi, ili kuwaonjesha wengine ile chemchemi ya upendo, furaha na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Hiki ndicho kiini cha wito wa kila mwamini. Kardinali Nichols anawaalika vijana kumkimbilia Kristo Yesu ili aweze kuwaosha na kuwatakasa kwa njia ya Damu yake Azizi na hatimaye, kuwakirimia maisha ya uzima wa milele!

Kwa upande wake Kardinali Antonio Canizares Llovera, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania amewaasa vijana kutambau na kujivunia kuwa ni sehemu ya Kanisa la Kristo katika maisha yao na kwamba, Kanisa linawapenda, linawaheshimu na kuwathamini. Linataka kuwajengea uwezo ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika haki, udugu, upendo na mshikamano wa dhati. Vijana wanapaswa kujisikia kuwa ni jeuri ya Kanisa na Jamii katika ujumla wale na wala hawana mbadala! Ni wajibu na dhamana ya Kanisa kuhakikisha kwamba, linayavalia njuga matatizo, changamoto na matumaini ya vijana wa kizazi kipya.

Ni wajibu wa Kanisa kuwatafuta na kuwasindikiza vijana waliopoteza imani na matumaini kwa kuchezea ujana wao na kusahau kwamba, fainali iko uzeeni, ili waweze tena kuandika historia ya maisha yao kwa imani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake! Vijana Barani Ulaya waoneshe moyo wa upendo na mshikamano kwa vijana wenzao wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora kwa kukimbia vita, kinzani, nyanyaso, umaskini na majanga asilia. Hawa ni wakimbizi na wahamiaji ambao kwa sasa wanakabiliana na changamoto kubwa za maisha Barani Ulaya.

Padre Michel Remery, Katibu mkuu msaidizi wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya amesema, Kongamano la Vijana Barani Ulaya lina mwangalia kijana na mahitaji yake msingi; changamoto, matatizo na furaha ya vijana wa Ulaya. Kanisa linapenda kuwasindikiza vijana katika hija ya maisha yao na kwamba, hata Kanisa halina budi kuwafunda viongozi watakaowasaidia vijana kufanya mang’amuzi ya wito katika maisha yao. Tukio hili linahudhuriwa pia na Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu ambaye amezungumzia kuhusu maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.