2017-03-29 09:35:00

Maaskofu DRC wajitoa katika mchakato wa utekelezaji wa mkataba wa 2016


Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC limejitoa katika mchakato wa usuluhishi wa mgogoro wa kisiasa nchini humo baada ya Mkataba wa Amani uliotiwa sahihi na Serikali ya Rais Joseph Kabila na Vuguvugu la Upinzani DRC kushindwa kutekelezwa kama ilivyokuwa imepangwa hapo tarehe 27 Machi 2017. Maaskofu wanasikitika sana kuona kwamba, juhudi zote zilizofanyika ili kurejesha tena utawala wa sheria na demokrasia ya kweli vinatoweka kama ndoto ya mchana, kiasi hata cha kuzua hofu na mashaka kuhusu mustakabali wa DRC kwa siku za usoni.

Askofu mkuu Marcel Utembi Tapa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC anasikitika kusema kwamba, wanasiasa wameshindwa kuonesha utashi wao wa kisiasa na kijamii kufikia muafaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa DRC. Matokeo yake, mkataba wa amani ambao ungesaidia mchakato wa maandalizi na hatimaye uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge kwa kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo ingeongoza kipindi hiki cha mpitoa kuelekea uchaguzi mkuu ambao ungefanyika mwishoni mwa mwaka 2017.

Uteuzi wa Waziri mkuu kutoka kwenye vyama vinavyounda vuguvugu la upinzani nchini DRC pamoja na usimamizi wa uchaguzi wa Rais na Wabunge. Mgawanyiko mkubwa miongoni mwa wapinzani ni chanzo kikuu cha kushindikana kwa utekelezaji wa mkataba wa amani uliokuwa ni matumaini ya wananchi wengi wa DRC.

Wakati huohuo, Baraza la Maaskofu Katoliki DRC limesikitishwa sana na mauaji ya kutisha yaliyofanyika hivi karibuni dhidi ya wanajeshi 50 waliokuwa wanatoka Tshikapa kuelekea Kananga. Mauaji haya yanasadikiwa kufanywa na Kikundi cha Waasi wa Kamuina Nsapu. Matukio kama yanaendelea kuhatarisha ulinzi, usalama, amani na umoja wa kitaifa ambao kwa sasa una hali tete sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.