2017-03-29 14:44:00

Jengeni umoja unaosimikwa katika utofauti ili kudumisha udugu na amani


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake Jumatano tarehe 29 Machi 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, alitambua kwa namna ya pekee kabisa uwepo wa wajumbe kutoka Iraq waliokuwa wanawawakilisha waamini wa madhehebu na dini mbali mbali waliokuwa wameambatana na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini. Baba Mtakatifu anasema, wajumbe hawa ni kielelezo na ushuhuda wa utajiri wa familia ya Mungu nchini Iraq wanaoonesha umoja katika utofauti, nguvu inayowaunganisha na kuwaimarisha katika ustawi, amani na maridhiano kati ya watu!

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea amani, umoja na mshikamano wa kitaifa nchini Iraq, ili nchi hii inayoundwa na waamini kutoka katika dini na madhehebu mbali mbali waweze kupata amani, umoja na maendeleo ya kweli. Baba Mtakatifu amechukua fursa hii kuwakumbuka watu ambao wamenaswa kwenye mashambulizi huko Mosul; wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha. Anasema, yuko pamoja nao kiroho! Anawataka wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuunganisha nguvu zao kulinda na kuwatetea raia, dhamana ambayo ni nyeti na kwamba, inapaswa kuvaliwa njuga mapema iwezekanavyo.

Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza katekesi yake, alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wajumbe kutoka Iraq waliokuwa wanawawakilisha waamini wa madhehebu na dini mbali mbali na kukazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kukuza na kudumisha utamaduni wa watu kukutana katika majadiliano ili kudumisha udugu na amani, kwani wote ni watoto wapendwa wa Mungu na kwamba, Ibrahimu ni baba yao wa imani. Kama ndugu wanapaswa kudumisha umoja kwa kutambua na kuthamini utofauti zao. Baba Mtakatifu amechukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapatia nafasi ya kuweza kumtembelea mjini Vatican, ili kuendeleza mchakato wa utajiri wa udugu na amani kwa ajili ya wote. Amani ambayo inapaswa kukita mizizi yake katika mioyo ya watu, nchini Iraq na amani duniani. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapatia wajumbe hawa baraka zake za kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.