2017-03-28 16:52:00

Jiaminisheni kwa Kristo ili awagange, awaponye na kuwapatia furaha!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 28 Machi 2017 amewataka waamini kumwamini Kristo Yesu katika maisha yao, ili waweze kutembea katika mwanga na furaha ya maisha badala ya kulalama katika dhambi. Baba Mtakatifu ameyasema haya kwa kurejea kwenye Injili ya Yohane 5:1- 6 inayomwonesha Yesu akimponya mgonjwa kiwete na aliyekuwa amepooza kwa muda miaka 38. Tukio hili anasema Baba Mtakatifu lilifanyika mjini Yerusalemu kwenye Birika la Bethzatha ambamo maji yake yalitumika kwa ajili ya kuwaponya wagonjwa mbali mbali.

Kulikuwa na mapokeo kwamba, maji haya yalikuwa yanachemshwa na Malaika na mtu wa kwanza kuingia ndani mwake alikuwa anaponywa magonjwa yake yote! Yesu kwa kumwona yule mgonjwa akamuuliza ikiwa kama alikuwa anapenda kupona na kuwa na furaha tena katika maisha kwa kujazwa na Roho Mtakatifu. Bila shaka wagonjwa wote waliokuwepo pale kama wangeulizwa na Yesu swali hili, jibu lao lingekuwa moja tu yaani “Ndiyo”. Lakini yule mgonjwa akamwambia Yesu kwamba, hakuna mtu anayemsaidia kuingia ndani pale maji yanapochemshwa na kwamba, kwa muda wa miaka 38 amejitahidi lakini bila mafanikio!

Mgonjwa huyu anasema Baba Mtakatifu ni sawa na mti uliopandwa pembeni mwa mto, lakini mizizi yake ilikuwa imenyauka kwani hakikuweza kufikia chemchemi ya maji ya uzima wa milele ili kupata afya. Mgonjwa yule hakuweza kukubaliana na hali yake ya ugonjwa akaanza kuwatupia wengine lawama. Haya ni matokeo ya dhambi kwa mtu kushindwa kuwajibika barabara na yale anayotenda; ni tabia ya kukata na kujikatia tamaa kiasi hata cha kutotamani wala kuthubutu kusonga mbele katika maisha. Ni mtu aliyepoteza kumbu kumbu ya furaha ya kweli katika maisha, kielelezo fika kabisa cha madhara ya dhambi yanayomnyima mtu furaha ya kweli kwa kudhani kwamba, hakutendewa haki katika maisha, hali inayonyong’onyeza roho ya mtu!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, licha ya mapungufu yote haya, Yesu anampatia furaha na matumaini kwa kumwambia “Simama, jitwike godoro lako uende! Akasimama, akajitwika godoro lake na kuanza kuchanja mbuga! Lakini, kwa bahati mbaya, ilikuwa ni Sabato, kiasi kwamba yule mgonjwa akaswalishwa maswali ili kufahamu ni nani aliyetenda tendo hilo kinyume cha Sheria ya Musa. Baba Mtakatifu anasema, yule mgonjwa hakupata hata nafasi ya kushukuru wala kumuuliza Yesu jina lake kutokana na furaha aliyokuwa nayo moyoni mwake.

Tabia ya kuishi kwa kuwatazama na kuwachunguza wengine inahatarisha maisha na kujikuta ukiwa kiwete, kiasi hata cha kushindwa kusimama na kutembea. Haya ndiyo madhara ya dhambi anasema Baba Mtakatifu, lakini Yesu, daima yuko tayari kuwasimamisha waja wake na kuwapatia ruhusa ya kutembea kifua mbele hata kama ni Siku ya Sabato. Yesu ni chemchemi ya maisha ya uzima wa milele inayozima kiu ya maisha ya wale wanaomtafuta Mungu kwa ari na moyo mkuu. Waamini wakionesha utashi wa kuponywa na Yesu, daima atawapatia neno la faraja, kiasi cha kusimama na kusonga mbele katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.