2017-03-27 08:49:00

Papa: Mwanga wa imani uwasaidie kupyaisha maisha yenu ya kiroho!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 26 Machi 2017 amesema, kiini cha Injili ya Jumapili ya IV ya Kipindi cha Kwaresima ni muujiza wa Yesu kumponya mtu aliyezaliwa kipofu, baada ya kupakwa tope na Yesu akaambiwa kwenda kunawa kwenye Birika la Siloamu na kurejea kwa Yesu huku akiwa anaona. Kwa njia hii, Yesu anajifunua kuwa kweli ni mwanga wa dunia, changamoto kwa waamini kutambua kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu, wanapaswa kumfahamu Mwenyezi Mungu.

Lakini, kutokana na uwepo pamoja na madhara ya dhambi, waamini wamegeuka kuwa vipofu, kumbe, wanahitaji mwanga wa imani unaotolewa na Kristo Yesu kama zawadi. Kipofu baada ya kuponywa upofu wake akamtambua Yesu na kumsujudia. Baba Mtakatifu anasema, hii ni safari ya imani kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu; imani inayofumbatwa katika maisha mapya yanayobubujika kutoka katika chemchemi ya Kisima cha Ubatizo, Sakramenti ya kwanza ya imani, inayomwezesha mwamini kuzaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu, tayari kuona na kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

Waamini wanaweza kugangwa na kuponywa upofu wao, ikiwa kama watakuwa na ujasiri wa kumtambua Kristo Yesu kuwa kweli ni mwanga wa Mataifa, tayari kumwambata na kufuata nyayo zake badala ya kuendelea kukandamizwa katika giza na utupu wa maisha. Kwa waamini waliopata bahati ya kuona na kutembea katika mwanga wa Kristo Yesu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanapaswa kutenda kama watoto wa mwanga, hali inayohitaji toba na wongofu wa ndani; upya wa maisha, mtazamo na kipimo cha kuwahukumu wengine kwa kuzingatia ngazi ya sifa zinazobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Ubatizo unawataka waamini kuishi na kutembea kama watoto wa Mwanga, changamoto endelevu inayotolewa na Kristo Yesu, mwenyewe! Ni mwaliko wa kumwamini na kumtumainia Kristo anayegeuza mioyo ya watu na kuwasaidia kuona kama anavyoona Yeye mwenyewe. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni mtazamo mpya tofauti kabisa na mtazamo wa kibinadamu unaoangalia mambo ya nje, lakini mtazamo wa Yesu unajikita katika mambo msingi ya maisha, yaani roho ya mtu! Huu ni mwaliko wa kuachana na mwanga unaopotosha; mwanga unaowasukuma watu kuwa na ubaridi na maamuzi mbele, kwa kuwahukumu watu pasi na huruma wala kuwapatia nafasi ya kujitetea.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kuwa, hii ndiyo hali ya kila siku ni sawa na “chakula cha kila siku” kwa watu wengi zaidi. Kwa wale wanaotembeza umbeya, watambue kwamba, wanaogelea katika giza la maisha ya kiroho na utupu! Mwanga mwingine ni ule unaowapeleka na kuwatumbukiza watu kwenye vishawishi na kuwahukumu watu wengine kadiri ya masilahi ya mtu binafsi. Ikiwa kama watu watawahukumu jirani zao kwa kujisikia na kwa kuzama katika mafao binafsi, watambue kwamba, wanatembea katika giza na wala ukweli haumo katika mahusiano na hali zilizopo. Kwa wale watu wanaofuata mafao binafsi, watambue kwamba, wanatembea katika uvuli wa giza na mauti!

Bikira Maria alikuwa ni mtu wa kwanza kumtambua Kristo Yesu kuwa ni mwanga wa Mataifa, awasaidie waamini kuupokea Mwanga huu wa imani katika kipindi hiki cha Kwaresima kwa kutambua na kuthamini zawadi ya Ubatizo ambayo wameipokea kutoka kwa Kristo Yesu. Mwanga mpya unaong’ara kutoka kwa Yesu, ulete mabadiliko makubwa katika maisha ya waamini ili kutoka katika umaskini na udhaifu wao, wawe kweli ni vyombo vya mwanga wa Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.