2017-03-27 14:35:00

Jengeni utamaduni wa kulinda na kutunza vyanzo vya maji!


Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Jumuiya ya Kimataifa ilipoanzisha Siku ya Maji Duniani, alipenda kutumia fursa hii kuwahimiza wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba wanasaidia kugaribisha umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji kwani maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu; ni rasilimali muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya binadamu; ni msingi wa mapambano dhidi ya umaskini na maradhi duniani. Aliwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kulinda na kuthamini uelewa na maana ya maji kadiri ya mapokeo ya dini na tamaduni mbali mbali za mwanadamu. Lakini kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu alikazia umuhimu wa kuwaelimisha vijana wa kizazi kipya utunzaji bora wa vyanzo vya maji, kwani maji ni rasilimali muhimu sana kwa binadamu wote!

Maadhimisho haya pia ilikuwa ni fursa ya pekee kwa Baraza la Kipapa la Utamaduni, Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kwa kushirikiana na Klabu ya Wananchi wa Argentina mjini Roma kuandaa kongamano kuhusu tunu ya maji kama njia ya kuzima kiu ya dunia! Wajumbe waliweza kufanya upembuzi yakinifu kuhusu umuhimu wa rasilimali maji kama sehemu ya haki msingi za binadamu inayodumisha utu na heshima ya binadamu.

Kardinali Peter Turkson, Rais Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu alisema, hii ni changamoto inayoihusisha Jumuiya ya binadamu, kwani ukosefu wa maji safi na salama ni hatari kwa utu, heshima, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu pamoja na mafao ya wengi. Rasilimali ya maji ni sehemu ya hali msingi ambayo kamwe hawezi mtu kuikosa kwa vile hana uwezo wa kulipia gharama zake. Inasikitisha kuona kwamba, hupatikanaji wa maji saji na salama si sawa sehemu mbali mbali za dunia, kwani taarifa za Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya milioni mia sita hawana fursa ya kupata maji safi na salama.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinakadiria kwamba, ifikapo mwaka 2050 idadi ya watu duniani inatarajiwa kufikia bilioni tisa. Lakini athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kusababisha ukame wa kutisha na mafuriko yanayosababisha maafa sehemu mbali mbali za dunia inakuwa ni changamoto kubwa katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote! Jumuiya ya Kimataifa isipokuwa makini anasema Baba Mtakatifu Francisko, watu watajikuta wanakinzana kwa sababu ya kugombania rasilimali maji.

Wazo ambalo limeungwa mkono pia na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican wakati akichangia mada kwenye kongamano hili. Hii ni changamoto pevu inayopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa anasema Askofu mkuu Paul R. Gallagher, kwa kushirikiana. Kwa upande wake, Silvia Zimmermann del Castillo, mwanzilishi wa Klabu ya Wananchi wa Argentina mjini Roma ameibua mbinu mkakati wa miaka mitano, utakaosimamia maendeleo ya sekta ya maji duniani, mkakati unaowaunganisha wadau kutoka sekta mbali mbali za maisha ili kusaidia kuendeleza mchakato wa uragibishaji wa maji kama sehemu ya haki msingi za binadamu.

Kampeni hii inawahusisha pia viongozi mbali mbali wa kidini kwa kutambua na kuheshimu kwamba, maji yanayo nafasi ya pekee katika ibada za dini mbali mbali duniani. Wote hawa wakiungana na kushikamana kwa dhati, wataweza kuunda mtandao wa ushirikiano kwa ajili ya kuhimiza utunzaji na matumizi bora ya rasilimali maji duniani. Kwa upande wake, Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni amekaza kusema, rasilimali maji ni muhimu sana katika maisha na Mapokeo ya dini mbali mbali duniani; maji ni chanzo cha majanga kwa binadamu, lakini maji pia ni chemchemi ya utakaso sanjari na maisha mapya! Kumbe, familia ya Mungu inawajibika kutunza vyanzo vya maji, ili kweli rasimali hii iweze kuwanufaisha watu wengi zaidi duniani na kamwe maji yasiwe ni chanzo cha vita na migogoro, bali kama sehemu ya haki msingi za binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.