2017-03-25 12:17:00

Kardinali Keeler alikuwa kweli ni Baba wa maskini!


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Kardinali William Henry Keeler aliyefariki dunia hapo tarehe 23 Machi 2017, akiwa na umri wa miaka 86. Baba Mtakatifu katika salam za rambirambi alizomwandikia Askofu mkuu William E. Lori wa Jimbo kuu la Baltimore anasema, anapenda kuungana na familia ya Mungu Jimboni humo kuomboleza kifo cha Kardinali Keeler aliyejitoa sadaka katika maisha na utume wake kama Askofu wa Jimbo Katoliki la Harrisburg na Bartimore; kama Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani kati ya mwaka 1992 – 1995. Ni kiongozi aliyejipambanua kwa ajili ya majadiliano ya kidini na kiekumene.

Baba Mtakatifu anapenda kuungana na wale wote wanaoomboleza msiba huu mzito, ili kuiombea roho ya Marehemu Kardinali Keeler, huruma ya upendo wa Baba wa Mbinguni. Baba Mtakatifu anapenda pia kutoa baraka zake za kitume na faraja kwa wale wote wanaoomboleza msiba huu mzito wakiwa na matumaini ya ufufuko na maisha ya uzima wa milele, ili roho ya Marehemu Kardinali Keeler iweze kupata pumziko la milele!

Itakumbukwa kwamba, Marehemu Kardinali William Henry Keeler alizaliwa kunako tarehe 4 Machi 1931, huko Texas, Marekani. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 17 Julai 1955. Baada ya Upadrisho alipangiwa kazi mbali mbali Jimboni mwake na baadaye kupelekwa Roma kwa ajili ya masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian na kujipatia shahada ya uzamivu kwenye Sheria za Kanisa kunako mwaka 1961. Wakati wa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican akiwa Katibu muhtasi wa Askofu George L Leech aliteuliwa Papa Yohane XXIII kati ya mwaka 1962 hadi mwaka 1965 kuwa mshauri maalum wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Tarehe 24 Julai 1979 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki la Harrisburg na kuwekwa wakfu kama Askofu tarehe 21 Septemba 1979. Tarehe 10 Novemba 1983 Papa Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Harrisburg. Tarehe 6 Aprili 1989 akateuliwa na Papa Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Baltimore na kusimikwa rasmi hapo tarehe 23 Mei 1989. Kati ya Mwaka 1992 hadi mwaka 1995 alikuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, NCCB. Katika maisha na utume wake kama : Padre, Askofu na hatimaye Kardinali, vipaumbele vya kwanza vilikuwa ni uinjilishaji na elimu inayojikita katika kanuni maadili na utu wema; akajitambulisha kuwa ni Baba wa maskini kwa kuwapatia watu makazi pamoja na kuzijengea uwezo familia sanjari na kuzisaidia zile familia zilizokuwa zinaogelea kwenye shida na mahangaiko makubwa: kiroho na kimwili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.