2017-03-24 14:42:00

Vita nchini Syria ni chanzo kikuu cha majanga kwa watu!


Vita ambayo imedumu nchini Syria kwa muda wa miaka sita imekuwa ni chanzo kikubwa cha maafa kwa watu na mali zao; familia zimesambaratika, miundo mbinu ya huduma na uzalishaji imeharibiwa vibaya sana; hakuna tena mahali pa sala na ibada kwa waamini; watoto wanaendelea kupoteza maisha kutokana na utapiamlo wa kutisha na kwamba, ujinga, magonjwa na umaskini vimeongezeka maradufu katika kipindi cha vita. Huu ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, nchini Uswiss wakati wa kuchangia kwenye mjadala kuhusu hali tete ya vita huko nchini Syria.

Ujumbe wa Vatican unapenda kuonesha mshikamano wake wa upendo kwa wananchi wote wa Syria walioguswa na kutikiswa na vita isiyokuwa na kichwa wala miguu kwa muda wote huu wa miaka sita. Hii inaonesha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujifunza kwa mara nyinge tena kwamba, vita si suluhu ya matatizo ya binadamu. Uchu wa fedha, mali na madaraka umepelekea mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia. Wafanyabiashara wanaotafuta faida kubwa inayonuka damu ya maskini, wamechuma kiasi kikubwa cha fedha na kusababisha watu zaidi ya milioni tano kukimbia Syria na kuanza kuishi uhamishoni.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, zaidi ya watu milioni 13.5 wanahitaji msada wa dharura na kwamba, makazi ya watu yamebaki kuwa ni magofu. Ujumbe wa Vatican unapongeza hatua ambayo imepatikana kwa siku za hivi karibuni kuhusu mgogoro wa kivita huko Syria, lakini unapenda kukumbusha kwamba, vita kamwe si suluhu ya migogoro ya kijamii, kwani madhara yake ni makubwa zaidi, lakini wanaotesa ni maskini, “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Malezi na makuzi ya watoto wengi yameathirika kutokana na vita. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hawa ni watoto ambao wamepokwa maisha ya utoto na ujana wao; wamenyimwa fursa ya kucheza kama watoto na kwenda shule ili kujipatia elimu, ujuzi na maarifa.

Ujumbe wa Vatican katika majadiliano kwenye Baraza Kuu la Haki Msingi za Binadamu la Umoja wa Mataifa unapenda kukazia pamoja na mambo mengine: umuhimu wa kujizatiti kutafuta na kudumisha amani; msamaha na upatanisho ili kuondokana na falsafa ya jino kwa jino; jicho kwa jicho! Madhara ya vita huko Syria ni kielelezo cha kushindwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika kuchuchumilia haki msingi za binadamu! Amani nchini Syria ni wajibu wa familia nzima ya binadamu na kwamba, tofauti za kidini, kiimani na kikabila kisiwe ni kisingizio cha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, bali ziheshimiwe kama tunu msingi za maisha ya kijamii, amana na urithi wa wengi. Jumuiya ya Kimataifa iendelee kujikita katika majadiliano yanayofumbata ukweli, uwazi na haki sawa kwa wadau wote, ili kuweza kutafuta mustakabali wa Syria na watu wake; kwa kukazia utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili hatimaye, kuondokana na tabia ya watu kutaka kulipiza kisasi. Wananchi wote wa Syria kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataufa wanawajibika kulinda, kutunza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.