2017-03-24 13:39:00

Umoja wa Ulaya Miaka 60: bado unahitajika na wengi!


Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, Alhamisi, tarehe 23 Machi 2017 ameongoza Ibada ya mkesha kwa ajili ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Ulaya kwa kusema kwamba, Kanisa linaamini kwamba, Jumuiya hii bado inahitajika sana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu ndani na nje ya Bara la Ulaya. Maaskofu kutoka Umoja wa Ulaya wanauangalia Umoja huu kwa umakini na matumaini makubwa.

Kardinali Bagnasco alitumia nafasi hii kwa ajili ya kusali na kuwaombea wahanga wote wa vitendo vya kigaidi vinavyondelea kupandikiza mbegu ya kifo, wasi wasi na woga miongoni mwa wananchi wa Jumuiya ya Ulaya. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni anasema Kardinali Bagnasco kumekuwepo na mashambulizi mengi ya vitendo vya kigaidi, kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Ulaya kuwekeza zaidi katika amani, ulinzi, usalama na maendeleo ya watu wake. Hii ni amana ambayo inapaswa kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali Barani Ulaya.

Kwa namna ya pekee, Kardinali Bagnasco anawaalika waamini kumwomba na kumkimbilia Kristo Yesu, Mfalme wa amani ili aweze kuwajalia amani, usalama, ustawi na utulivu wa ndani kwa njia ya mwanga wa Roho Mtakatifu. Mwanga huu unapatikana kwa kuutafuta kwa juhudi na maarifa. Viongozi wa Jumuiya ya Ulaya wanapaswa kuchachuliwa kwa mwanga na tunu msingi za maisha ya Kiinjili, kwa kufumbata kwa namna ya pekee kabisa fadhila ya unyenyekevu, hekima na imani.

Kardinali Bagnasco anakaza kusema, Kanisa Katoliki kwa kushirikiana na Makanisa mengine yanapania kuchangia kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu ndani na nje ya Jumuiya ya Ulaya, kwa kuheshimiana, kuaminiana, kushirikiana na kushikamana. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Ulaya kurejea tena kwenye asili yake inayopata chimbuko kwenye tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Kwa njia hii, Umoja wa Ulaya utaweza kustawi kama mtende wa Lebanon, kwani chachu ya Kiinjili kamwe haiwezi kupitwa na wakati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.