2017-03-23 15:40:00

Rais Paul Biya wa Cameroon akutana na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 23 Machi 2017 amekutana na kuzungumza na Rais Paul Biya wa Cameroon ambaye alikutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican. Baba Mtakatifu na mgeni wake katika mazungumzo yao ya faragha wameridhishwa na uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Cameroon sanjari na mchango wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Cameroon, hususan kwenye sekta ya elimu na afya. Wameridhishwa na amani na utulivu unaoshuhudiwa na familia ya Mungu nchini Cameroon licha ya tofauti zao za kidini na kikabila.

Viongozi hawa wawili wamekazia umuhimu wa kusimama kidete kujenga na kudumisha mafungamano ya kijamii kwa kuendeleza amana na mapokeo ya wananchi wa Cameroon; sanjari na kusimamia haki msingi za binadamu na zile za makundi ya watu wachache ndani ya jamii. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko na Rais Paul Biya wa Cameroon wamebadilishana mawazo kuhusu tema mbali mbali zinazogusa masuala ya kimataifa, lakini muhimu zaidi yale yanayogusa Ukanda wa Bara la Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.