2017-03-23 14:05:00

Kumbu kumbu ya miaka 60 ya Jumuiya ya Bara la Ulaya! Changamoto zake!


Ilikuwa ni tarehe 25 Machi 1957 mjini Roma, viongozi wakuu kutoka Ubelgiji, Ufaransa, Italia, Luxembourg, Netherland na Ujerumaini ya Mashariki wakati ule, zilipotia sahihi Mkataba wa Roma na huo ukawa ndio mwanzo wa Jumuiya ya Uchumi Barani Ulaya, ambayo kwa sasa inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 60 tangu kuanzishwa kwake! Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni tarehe 24 Machi 2017 anatarajiwa kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya na kilele chake ni Jumamosi, tarehe 25 Machi 2017 hapa mjini Roma. Kutakuwepo na Mkesha wa Sala ya Kiekumene kwenye Kanisa kuu la Watakatifu wote Jimbo kuu la Roma.

Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, CCEE anasema, huu ni wakati muafaka kwa viongozi wakuu wa Jumuiya ya Uchumi Barani Ulaya kufanya upembuzi yakinifu ili kugundua tunu msingi zilizowasukuma waasisi kuanzisha Umoja huu. Wawe na ujasiri wa kurejea tena kwenye tunu msingi za Umoja huu. Bila utambulisho makini, Umoja wa Uchumi Barani Ulaya hauna maisha marefu kama hali inavyojionesha kwa baadhi ya nchi kutaka kujiuengua kutoka kwenye Umoja huu kama ilivyofanya Uingereza!

Kardinali Bagnasco anasema, kama sehemu ya maadhimisho haya amepata nafasi ya kuzungumza na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli pamoja na Patriaki Cyril wa Moscow na Russia nzima. Hawa ni viongozi wenye karama, wanaendelea kuwaongoza waamini wao kwa imani na upendo kwa Kristo na Kanisa lake. Wanaziona changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa,  ndio maana wanakazia kwa namna ya pekee: Uekumene wa huduma, sala na damu kama kielelezo cha ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake. Wakristo wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi kwa njia ya mshikamano wenye mvuto na mashiko!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza amekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo Barani Ulaya. Anawataka waamini kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika vitendo vya kigaidi pamoja na kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Waamini wanapaswa kusaidiwa kujenga Injili ya upendo kwa Mungu na jirani zao, kwa kusaidiana, kwani Mungu ni upendo na chemchemi ya amani na utulivu wa ndani, mambo ambayo watu wanayahitaji sana Barani Ulaya, ukizingatia kwamba, kwa sasa hofu ya mashambulizi ya kigaidi imetanda sehemu mbali mbali za Umoja wa Ulaya.

Kumbe, kumbu kumbu ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya iwe ni fursa kwa viongozi wa Bara la Ulaya kuchunguza dhamiri ili kurejea tena katika tunu msingi za Umoja wa Ulaya; kusoma tena historia ya maisha na watu wake; kugundua tena na tena utambulisho wake ili kuuendeleza kwa ari na moyo mkuu. Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kamwe haiwezi kujengwa na kusimikwa tu kwenye masuala ya fedha na uchumi, kwa kufanya hivi, itapoteza dira na mwelekeo wa maisha. Ni wakati wa kuangalia ikiwa kama katika kipindi cha miaka 60 wamekuwa waaminifu kwa ndoto ya waasisi wa Umoja wa Ulaya. Ni wakati muafaka wa kuangalia tena, Je, ubinafsi na utaifa usiokuwa na mashiko wala mvuto chanzo chake nini? Tabia ya ukanimungu, ubaridi wa imani pamoja na watu kutukuza na kumezwa mno na malimwengu, imepelekea watu kumezwa na ubinafsi na matokeo yake ni hizo cheche za Uingereza kujiengua kutoka kwenye Umoja wa Jumuiya ya Ulaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.