2017-03-22 13:00:00

Siku ya Maji Duniani 2017 na changamoto zake!


Jumuiya ya Kimataifa tarehe 22 Machi 2017 inaadhimisha Siku ya Maji Duniani, huku kukiwa na taarifa kwamba, kuna watu zaidi ya bilioni moja ambao hawana maji safi na salama, hali ambayo inahatarisha ubora wa maisha na afya zao. Waathirika wakuu ni watu wanaoishi: Barani Asia, Afrika na Amerika ya Kusini kadiri ya taarifa iliyotolewa na Baraza la Maji Duniani. Ukosefu wa maji safi na salama unaigharimu Jumuiya ya Kimataifa kiasi cha dola za kimarekani bilioni 500 kwa kila mwaka.

Watu wanaoishi katika nchi maskini wanatumia kiasi kidogo sana cha maji ikilinganishwa na wale wanaoishi katika nchi tajiri zaidi duniani. Licha ya uhaba wa maji safi na salama sehemu mbali mbali za dunia, Shirika la Afya Duniani, WHO linasema, kuna mamilioni ya watu wanaoteseka kutoka na mafuriko au ukame wa kutisha uliosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinahatarisha pia uhakika na usalama wa chakula duniani. Nigeria, Sudan ya Kusini, Somalia na Yemen kwa sasa ni nchi ambazo zinakabiliwa na baa la njaa na kwamba, zinahitaji msaada wa dharura.

Kwa upande wake, Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO linasema uharibifu mkubwa wa mazingira ni hatari sana kwa maisha ya binadamu kwani hadi sasa asilimia kubwa ya watu duniani wanatumia misitu kama malighafi kwa shughuli za uzalishaji na huduma pamoja na kuwa ni fursa ya ajira kwa watu wengi. Uharibifu mkubwa wa mazingira ni chanzo cha mafuriko na ukame wa kutisha inasema FAO.

Maji ni sehemu muhimu sana kwa maisha, ustawi na maendeleo ya binadamu, changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kusimama kidete ili kujenga utamaduni wa utunzaji bora wa maji, kwani maji ni uhai ikiwa kama ubora na usalama wake utazingatiwa na wote. Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu ana haki ya kupata maji safi, salama na yenye ubora! Binadamu anapaswa kujifunza kutumia rasilimali maji kwa unyenyekevu bila kuyachafua. Haki ya maji safi na salama ni kati ya changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba kuna baadhi ya nchi ambazo bado hazijatambua kwamba, maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na baadhi ya nchi zinapinga maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Rasilimali maji inapaswa kushughulikiwa kikamilifu kwani hii ni sehemu muhimu sana katika mchakato wa maboresho ya maisha ya binadamu sanjari na mapambano dhidi ya umaskini duniani.

Baraza la Maji Duniani linapenda kuwahamasisha viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanayavalia njuga matatizo na changamoto zinazofumbatwa katika rasilimali maji, ili kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi duniani wanakuwa na uhakika wa kupata maji safi na salama, kwa ajili ya matumizi ya binadamu na maendeleo yake endelevu. Takwimu zinaonesha kwamba, ni asilimia 12% ya idadi ya watu wote duniani ndiyo inayofaidika kwa kupata huduma ya maji safi na salama duniani. Zaidi ya watu milioni 3. 5 wanafariki dunia kila mwaka kutokana na magonjwa yanayohusishwa na matumizi ya maji yasiyo safi wala salama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.