2017-03-22 13:30:00

Majadiliano ya kidini ni shule ya amani, udugu na maendeleo ya wengi


Majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali ni muhimu sana katika ujenzi wa misingi ya haki, amani, maridhiano, upendo na mshikamano wa dhati, dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika vita, vitendo vya kigaidi na nyanyaso na dhuluma sehemu mbali mbali za dunia. Kila dini inazo tunu msingi za maisha ya kiroho zinazoweza kushirikishwa kwa waamini wa dini nyingine, ili kutengeneza dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa kujikita katika misingi ya: haki, udugu na maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili.

Huu ni mchango ambao umetolewa hivi karibuni na Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, wakati alipokuwa anashiriki kwenye mkutano wa tano wa kimataifa uliokuwa umeandaliwa na Kituo cha Kimataifa cha Dini ya Kiislam kuhusu Sheria na Maadili, huko Doha, Falme za Kiarabu.  Askofu Guixot amechambua kwa kina na mapana kuhusu kinzani na ukosefu wa kanuni maadili; Vita vya kidini maarufu kama Jihad na “Vita ya Haki”.

Dhana ya vita ni changamoto pevu katika maisha ya binadamu, kumbe, hapa jambo la msingi kwa waamini wa dini mbali mbali ni kushrikiana na kushikamana pamoja na watu wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho. Anakaza kusema, majadiliano ya kweli ya kidini yanafumbatwa katika umoja na udugu; urafiki na ushirikiano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Ni kutokana na mwelekeo kama huu, majadiliano ya kidini yanaweza kujenga shule ya ubinadamu na chombo cha umoja, upendo na mshikamano, ili kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya binadamu.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na viongozi wakuu wa Kanisa waliofuatia baadaye, lakini zaidi Baba Mtakatifu Yohane Paulo II hadi kwa Papa Francisko wamekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam. Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki inafafanua vyema kuhusu uhusiano wa Kanisa na Waislam kwa kusema kwamba “mpango wa wokovu unawakumbatia pia wale wanaomkiri Muumba, na kati ya hawa mahali pa kwanza ni Waislam wanapokiri imani ya Ibrahim, wanamwabudu pamoja na Wakristo, Mungu aliye mmoja tu, mwenye huruma na atakayewahukumu watu siku ya mwisho.

Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot anasikitika kusema kwamba, misimamo mikali ya kidini na mashambulizi ya kigaidi ni changamoto kubwa na hatari kwa: amani, usalama, haki msingi za binadamu na mafungamano ya kijamii. Ni vitendo ambavyo vinapandikiza mbegu ya chuki na uhasama kati ya watu. Ikumbukwe kwamba, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ni mambo ambayo kamwe hayawezi kufumbatwa kwenye kanuni maadili na maisha ya kiroho. Haki, amani, upendo na mshikamano vinaweza kukua na kukomaa, ikiwa kama waamini wa dini mbali mbali wataweza kushirikiana na kushikamana kwa dhati kama ndugu kwa njia ya majadiliano ya kidini. Waamini wabadilike badala ya kuendekeza sheria zilizopindishwa kwa ajili ya mafao ya watu wachache, ili kukoleza mchakato wa majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.