2017-03-22 13:30:00

Macho yetu DRC, 27 Machi 2017


Askofu mkuu Fridolin Ambongo, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki DRC anasema, familia ya Mungu nchini humo inajiandaa kwa ajili ya kushuhudia utiwaji wa sahihi kati ya Serikali na Vuguvugu la upinzani “Rassemblement” ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hapo tarehe 27 Machi 2017, tayari kuanza mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika katika kipindi cha mwaka 2017 ili kuonesha ukomavu wa kidemokrasia. Baraza la Maaskofu Katoliki DRC limekuwa ni mpatanishi wa Serikali na Vuguvugu la upinzani kiasi cha kuyawezesha makundi haya mawili kutia sahihi kwa mkataba wa amani hapo tarehe 31 Desemba 2016.

Askofu mkuu Fridolin Ambongo anasema, hadi sasa kazi kubwa imekwisha kutekelezwa katika mikutano elekezi iliyofanyika katika siku za hivi karibuni na wadau wakuu kushirikishwa yale yaliyofikiwa kwenye mkutano huu. Rais wa Baraza la Umoja wa Kitaifa anapaswa kuhakikisha kwamba, anasimamia utekelezaji wa makubaliano ya mkataba wa kati ya Serikali na Vuguvugu la upinzani, uliotiwa sahihi hapo tarehe 31 Desemba 2016.

Dhamana ya kuratibu utekelezaji wa makubaliano ya mkataba wa amani alikuwa apewe Etienne Tshisekedi, lakini akaaga dunia mapema hata kabla ya utekelezaji wa mktaba wa amani kuanza nchini DRC. Vyama vingine vya upinzani vinasema, nafasi hii inapaswa kuangaliwa upya. Kimsingi Waziri mkuu kadiri ya makubali ya mkataba wa amani nchini DRC anapaswa kutoka katika  Vugu vugu la upinzani wakati ambapo Rais Joseph Kabila ataendelea kushikilia wadhifa wake kama Rais wa nchini. Changamoto hii kwa sasa inavaliwa njuga, ili ifikapo tarehe 27 Machi 2017, kiwe kimeeleweka kwa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.