2017-03-18 16:34:00

Mwenyeheri Josef Mayr-Nusser, shuhuda wa uaminifu kwa Kristo!


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Jumamosi tarehe 18 Machi 2017, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amemtangaza Mtumishi wa Mungu Josef Mayr Nusser aliyafariki dunia kunako mwaka 1945 kuwa ni Mwenyeheri. Katika maisha yake, aliwahi kuwa ni Rais wa Chama cha Vijana Wakatoliki Italia, akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii hasa baada ya kipindi kigumu cha Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa Jimboni Bolzano, Italia.

Alikuwa pia ni mwanachama wa Chama cha Mtakatifu Vincent wa Paulo kwa ajili ya kuwahudumia maskini. Kwa njia hii, aliweza kumtambua na kumhudumia Kristo Yesu aliyejidhihirisha miongoni mwa maskini. Alikuwa ni mwamini thabiti katika maisha na imani yake kwa Kristo Yesu kiasi cha kukataa kula kiapo cha utii kwa Adolf Hitler. Padre Josef Innerhofer aliyekuwa anashughulikia mchakato wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Nusser kuwa Mwenyeheri anakaza kusema, Mwenyeheri mpya kweli alishuhudia imani yake kwa Kristo na Kanisa lake katika medani mbali mbali za maisha: ndani ya familia, sehemu za kazi na hata alipokuwa kwenye mapumziko, hakuwa ni mtu wa “kujirusha sana na malimwengu”!

Mwenyeheri Josef Mayr Nusser alikataa kula kiapo cha utii kwa Hilter kwa sababu ya siasa na sera zake za kibaguzi zilizokuwa zinadhalilisha utu na heshima ya binadamu; kinyume kabisa cha tunu msingi za Kiinjili. Hakuogopa kifo hata baada ya kutishwa kwamba, angemwacha mke wake akiwa mjane na mtoto wao akiwa yatima, lakini alikaza kusema, ataendelea kuwa mwaminifu hadi dakika ya mwisho bila kujali kifo. Aliuwawa kikatili huku akiwa amevalia Rozari Takatifu, akiwa na Misale ndogo pamoja na Kitabu cha Agano Jipya, utajiri peke aliokuwa amebaki nao wakati wa kukabiliana na mauti!
Mwenyeheri Josef Mayr Nusser ni mfano bora wa kuigwa katika kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake hadi tone la mwisho la maisha pasi na kuogopa! Waamini wanapaswa kuwa macho na matukio mbali mbali yanayotendeka duniani, ili kuimarisha imani pamoja na kuwa tayari kuishuhudia hata kama watapaswa kutoa sadaka kubwa. Kwa maneno mengine, Wakristo wanapaswa kuwa tayari kutoa maamuzi mazito katika maisha yao!


Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.