2017-03-17 10:54:00

Waungamishaji wawe: Marafiki wa Yesu, Mashuhuda na Wainjilishaji


Padre muungamishaji anayejisadaka kwa ajili ya kuwaonjesha waamini huruma ya Mungu ni rafiki mwema wa Yesu, Mchungaji mwema; ni chombo na shuhuda wa Roho Mtakatifu na kwamba, kiti cha maungamano ni mahali muafaka pa Uinjilishaji, unaomwezesha mwamini kukutana na huruma ya Mungu katika maisha yake; huruma ambayo imefunuliwa kwa njia ya Uso wa Kristo Yesu. Huu ni muhtasari wa hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 17 Machi 2017 alipokutana na kuzungumza na wajumbe 700 waliokuwa wanashiriki katika mafunzo ya ndani ya wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, yaliyoanza hapo tarehe14 - 17 Machi 2017 mjini Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Idara ya Toba ya Kitume ni mahakama ya huruma ya Mungu inayogusa kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Ni mahakama inayomwezesha mwamini kupata dawa ya maisha yake ya kiroho kutoka katika huruma ya Mungu. Majiundo makini kwa waungamishaji wema ni muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa kwa nyakati hizi. Hii ni changamoto kwa wahudumu na vyombo vya huruma ya Mungu kujikita katika malezi endelevu katika maisha yao, ili huduma hii iweze kuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wao.

Kwanza kabisa Padre muungamishaji bora ni yule ambaye anajenga na kudumisha uhusiano mwema na Kristo Yesu, mchungaji mwema kwa njia ya sala inayomwilishwa katika upendo wa shughuli za kichungaji ili kuwasindikiza waamini wanaokimbilia kiti cha huruma ya Mungu katika maisha yao. Mhudumu wa huruma ya Mungu anayejikita katika maisha ya sala atakuwa mwangalifu  na makini wakati wa kuadhimisha Ibada ya Sakramenti ya Upatanisho. Padre muungamishaji ni mtu anayetambua kwamba, kabla ya kuwaungamisha wadhambi wengine, yeye ni mdhambi wa kwanza aliyesamehewa dhambi zake, ili kuwashirikisha wengine huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Sala inamnyenyekesha na kumlainisha muungamishaji, ili aweze kutoa hukumu ya haki kwa dhambi zilizotengwa sanjari na kuonesha huruma kwa mdhambi anayekimbilia ili kuambata huruma ya Mungu katika maisha yake.

Katika sala, Padre muungamishaji atambue moyoni mwake majeraha na madonda yanayosababishwa na dhambi, ili kwa unyenyekevu mkubwa aweze kuwaganga na kuwaponya wale wanaoteseka kutokana na dhambi kwa mafuta ya huruma ya Mungu kama alivyofanya Msamaria mwema kwa yule mtu aliyevamiwa na wanyang’anyi kule Yeriko wakamtenda vibaya kiasi cha kumwacha karibu ya kufa! Katika Sala wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu waombe fadhila ya unyenyekevu, ili waweze kutenda kadiri ya mapenzi ya Yesu kwa kuwahuruma watu wake. Katika Sala wamwombe Roho Mtakatifu awakirimie roho ya huruma na mang’amuzi, ili kutambua mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu wanaokimbilia kiti cha huruma na upendo wa Mungu ili kugangwa na kuponywa na umaskini wa dhambi!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Padre muungamishaji mahiri ni chombo na shuhuda wa Roho Mtakatifu anayemkirimia paji la mang’amuzi linalofumbatwa katika utamaduni wa kusikiliza kwa makini Roho Mtakatifu na kuwa tayari kutenda mapenzi ya Mungu. Kukosekana kwa karama hizi kunalitendea sana Kanisa na waamini wanaokimbilia huruma ya Mungu katika maisha yao. Padre muungamishaji anapaswa kutekeleza mapenzi ya Mungu; kufundisha kila ambacho Kanisa linafundisha, daima akiwa ameungana na Kristo na Kanisa lake na wale si vinginevyo! Padre akumbuke kwamba, ni mhudumu wa Sakramenti ya Upatanisho.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mang’amuzi yanamwezesha Padre muungamishaji kuwa na malezi makini ili kuangalia mambo na moyo wa mtu kwa kuthamini utakatifu wa dhamiri ya mwanadamu ili aweze kupata mwanga, amani na huruma ya Mungu. Mang’amuzi makini ni msaada mkubwa kwa waamini wanaoteseka kwa dhambi; kumbe, hapa kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu ili hatimaye, kumsaidia mwamini kuganga na kuponya yale mambo msingi katika maisha yake ya kiroho. Pale ambapo afya ya akili iko mashakani, kuna haja kwa wahusika kuhakikisha kwamba, wanashirikiana na sayansi ya tiba ya mwanadamu pamoja na wale ambao wamekabidhiwa dhamana na Jimbo ili kuwapunga watu pepo wachafu!

Baba Mtakatifu anasema, kiti cha maungamo ni uwanja makini wa Uinjilishaji wa kweli unaomwezesha mwamini kukutana na kuambata huruma ya Mungu katika maisha yake; Uso wa huruma ambao umefunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu. Hapa ni mahali pa majiundo endelevu katika maisha ya kiroho yanayofumbatwa katika mambo msingi ya kiimani; kwa kutangaza Neno la Mungu linalokumbatiwa kwa namna ya pekee upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake. Ni mahali muafaka pa kumwelekeza mwamini mambo msingi ya maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu, kwa kuzingatia ukweli, mafao ya mwamini sanjari na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha. Hapa ni mahali muafaka pa kutumia vyema paji la akili ili kufanya mang’amuzi ya busara yatakayowasaidia waamini katika maisha yao.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anahitimisha kwa kusema, Padre muungamishaji daima anahamasishwa kila siku kutoka na kwenda pembezoni mwa dhambi na ubaya na kwamba, kipaumbele chake cha kwanza ni sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Kumbe, waungamishaji wema na watakatifu ni wale wanaojisadaka kila siku ili kujenga uhusiano wao na Kristo Yesu kwa njia ya sala; watu wanaoweza kufanya mang’amuzi ya kina kwa msaada wa Roho Mtakatifu na tayari kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.