2017-03-17 09:34:00

Roho Mtakatifu anawasaidia waamini kumfahamu Kristo, Mungu kweli!


Padre Raniero Cantalamessa mhubiri wa nyumba ya kipapa anasema, kauli mbiu inayoongoza tafakari za kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2017 “Hawezi mtu kusema Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu”. (Rej. 1 Kor. 12: 3) na kwamba, Roho Mtakatifu anawasaidia waamini kuweza kumfahamu vyema Kristo “ Mungu aliyetoka kwa Mungu”, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kristo Yesu ndiye aliyeushinda ulimwengu na ni mwanga wa mataifa. Wanaheri wale wanaolifahamu fumbo la maisha na kifo ndani ya Kristo!

Kimsingi haya ndiyo mawazo makuu yaliyojitokeza wakati wa Mahubiri ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima yaliyotolewa na Padre Raniero Cantalamessa, Ijumaa tarehe 17 Machi 2017 kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko, viongozi waandamizi kutoka Vatican pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume yaliyoko mjini Roma. Kuna makundi mbali mbali ya watu wanaomwamini Yesu kuwa ni Kristo, Masiha na Mkombozi wa ulimwengu, kazi na dhamana ambayo inafanywa na Roho Mtakatifu, anayewawezesha waamini hawa kupata maana kamili na uhusiano wa ndani na Kristo Yesu.

Kanisa katika Kanuni ya Imani ya Nicea ya Mwaka 325 linaungama kwamba, Yesu Kristo ni Bwana “Aliyezaliwa bila kuumbwa, wenye umungu mmoja na Baba, ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Huu ni mchango mkubwa uliotolewa na Mtakatifu Athanasi wakati wa mkutano wa Nicea kama ungamo la imani mintarafu Umungu wa Kristo dhidi ya uzushi uliokuwa umetolewa na Arius aliyekuwa anapinga Umungu wa Kristo. Kanuni ya imani inakaza kusema, Yesu alizaliwa bila kuumbwa “ genitus non factus”. Kumbe, tangu wakati huo, Yesu Kristo akaendelea kuungamwa kama Mungu aliyetoka kwa Mungu, Mwanga kwa Mwanga aliyezaliwa bila kuumbwa! Padre Cantalamessa anasema, hii ni kazi ya Roho Mtakatifu na kwamba, wokovu wa ulimwengu unafumbatwa katika Umungu wa Kristo.

Umungu wa Yesu Kristo ni kiini cha imani ya Kikristo inayofumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na Fumbo la Umwilisho, yaani Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwake yeye Bikira Maria; akazaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huyu ndiye Yesu anayeendelea kukaa kati pamoja na watu wake. Changamoto kubwa kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanashuhudia imani yao kwa Kristo Yesu kwa njia ya matendo yenye mvuto na mashiko! Kuenea kwa ukanimungu na kutopea kwa imani katika nchi zilizokuwa na utamaduni wa Kikristo ni mwaliko wa kuimarisha imani zaidi kwa njia ya katekesi makini. Imani ya Kikristo inafumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Mitume baada ya kushukiwa na Roho Mtakatifu siku ile ya Pentekoste, wakaimarishwa katika imani yao, kiasi hata cha kuthubutu kuiungama hadharani. Mtakatifu Paulo anasema kwa maana kwa moyo wa mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu na kadiri ya Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa imani inabubujika kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu! Mchakato wa Uinjilishaji mpya unapania kuwasaidia waamini kumfahamu vyema Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai, aliyeushinda ulimwengu, yaani Kristo aliyeshinda dhambi, kifo na mauti kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Kwa njia hii, Yesu amekuwa ni mwanga unaoangaza giza la maisha ya waamini na chanzo cha maisha mapya. Yeye ni mwanzo na mwisho, ni alfa na omega, nyakati zote ni zake. Yesu ni njia, ukweli na uzima. Yesu ni mwamba na nguzo thabiti ya maisha ya waamini wake.

Padre Raniero Cantalamessa anakaza kusema, Uinjilishaji mpya unakwenda sanjari na ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kama kielelezo cha utambulisho wao katika ulimwengu mamboleo. Wakristo wamebarikiwa kwani wanayo bahati ya kulifahamu fumbo la maisha na kifo wanalolishiriki na Kristo Yesu, mwenyewe anayewakirimia furaha isiyokuwa na kifani. Yesu ni chemchemi ya imani na furaha kwa waja wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.