2017-03-17 15:26:00

Kristo Yesu ni chemchemi ya maji ya uzima wa milele!


Baba Mtakatifu Francisko anasema maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na inaendelea kuwa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa. Ikiwa kama suala zima la maji halitashughulikiwa kikamilifu, kwa siku za usoni, linaweza kuwa ni chanzo kikuu cha kinzani na migogoro ya kimataifa. Maji safi na salama ni muhimu sana katika mchakato mzima wa maboresho ya afya ya binadamu. Ndiyo maana tunakutana na misemo kama “maji ni uhai”. Na pia mahali panapokosekana maji huwa panakosa amani kudhihirisha umuhimu wa bidhaa hii kwa maisha ya mwanadamu. Ukame wa maisha ya kiroho kwa upande mwingine hutunyima maji ya kiroho na hivyo kuupoteza uhai kiroho. Dominika hii ya tunaalikwa kumwelekea Mungu ili kupata maji ya uzima wa roho zetu na kuwa tena hai kiroho na kimwili.

Uwepo wa uovu duniani unafahamika na Mungu wetu. Tangu mwovu aipande mbegu ya uovu Mwenyezi Mungu alitangaza wazi nia yake ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika kongwa la utumwa wa shetani akisema: “nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake” (Mw 3:15). Uovu unaondoa uhai wetu kiroho na hivyo kunakuwa na ukame na utupelekea kuwa na kiu ya daima ya kumtafuta Mungu. Hivyo mwanadamu anapaswa kumwelekea Mungu ili kumkomboa kama anavyotualika mzaburi katika wimbo wa mwanzo wa dominika hii akisema:”Macho yetu humwelekea Bwana daima, naye atanitoa miguu yangu katika wavu”.

Tukiendelea na wazo letu la dominika iliyopita kwamba maisha ya kiroho ni safari, tunaona muunganiko na dominika hii ya leo kwamba, mbali na safari hiyo kutufikisha katika utukufu wa Mungu kama tulivyohitimisha katika dominika hiyo lakini pia inatupatia uhai wa kimungu. Tunakuwa hai katika Mungu na hivyo utukufu wake unamiminika kutoka ndani mwetu. Tendo la toba linatuletea uhai huo. Kwa tendo hili la toba tunapata fursa ya kuchota maji kutoka katika visima vya wokovu. Majira ya Kwaresima ni fursa kwetu ya kuuishwa tena na kuupokea uzima wa kimungu unaopotezwa na dhambi.

Kitabu cha kutoka kinatuelezea jinsi taifa la Israeli lilipokuwa safarini kutoka utumwani Misri. Simulizi hili linawaonesha wakiwa na mioyo migumu na kukatishwa tamaa na safari hii. Mara nyingi wana wa Israeli walipokuwa wanapatwa na makwazo wawapo njiani katika safari yao kurejea katika nchi yao ya ahadi walirejea kukumbuka mapochopocho ya utumwani Misri bila kujali kwamba walibaki kuwa fikra za kitumwa na hadhi yao kugaragazwa chini. Hali hii ndiyo anayokuwa nayo mdhambi. Yeye ambaye amelowea katika utamu wa maisha ya kidunia anapoanza kufunga na kujisadaka kwa ajili ya kurejea katika uhuru wa kweli hukatishwa tamaa na ugumu wa safari. Hivyo hukosa hamu na ladha ya maisha na kujiona kana kwamba ameachwa jangwani kuangamia.

Ugumu wa mioyo kwa mwanadamu kama ilivyokuwa zamani hizo za Musa hujitokeza hata katika nyakati zetu hizi. Jambo la kututia moyo ni uwepo wa “Musa” ambaye tunapomnung’unikia kwa kudhani yeye ndiye ametukengeusha basi hutenda kama mkaakati na kuturudishia tena matumaini: “Musa akamililia Bwana, akisema, Niwatendee nini watu hawa? Bado kidogo nao watanipiga mawe”. Kilio hiki kinamfikia Mungu na anatenda. Nafasi hii ya Musa inawakilishwa na uwepo wa Kanisa ambalo linatupatia majira haya kwa ajili ya kuuonja upendo wa Mungu na kupata tena uhai wa kimungu. Hivyo ni majira ambayo yanatuita kuinua macho yetu ya ndani, yaani macho yetu ya kiroho na kuziona fadhili za Mungu; kuinua macho yetu na kuchota maji kutoka kisima cha wokovu.

Tunapouonja upendo wa Mungu kupitia njia mbalimbali au kwa kupitia fadhili mbalimbali anazotukirimia huwa tunaugundua upotovu wetu na kujiunga naye karibu zaidi. Mwanamke Msamaria anaanza kwa kuonesha ubora na umwamba wa mapokeo yao: “Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria?”. Kiutamaduni hawakuungana wala kuchangamana na ukamilifu ulionekana katika kulitimiliza hilo. Upendo wa ndugu ulijengewa mipaka lakini upendo huu ulikuwa mubashara bila hata chenga ni wa kibinadamu. Mwanamke huyu ambaye anawawakilisha wenzake walikuwa bado hawajauonja upendo wa kimungu.

Jibu la Kristo “kama ungalijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angekupa maji yaliyo hai” linaanzisha safari ya mageuzi kwa mwanamke huyu Msamaria. Jibu hili linamgutusha na kuanza safari ya kumgeukia Mungu kusudi apate uzima. Uhai anaonuia Kristo si uhai huu wa kimwili kama analivyoelewa yule mama bali ni uzima wa kimungu ambao unamfanya mmoja kuwa hai daima: “Yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujika uzima wa milele”.

Hili ni dokezo la safari ya kiroho ambayo kwayo mwanadamu atatoka katika giza na utumwa wa shetani na kwenda katika mwanga na kuwa wana warithi wa Mungu. Tofauti na Waisraeli katika somo la kwanza la dominika hii ambao walikatishwa tamaa na kuanza kulalama kwa sababu ya kiu ya kimwili Kristo anatualika kuanza kuona kiu ya kiroho; kukereka ndani rohoni kwa kukosa kuuonja upendo wa Mungu na kushindwa kuusambaza upendo huo kwa wengine kusudi sote tuuonje uhai huo wa kimungu. Tunaalikwa kujitambua jinsi tunavyokosa kuwa na upendo kwa Mungu na kwa wenzetu, kuangalia jinsi tunavyoshindwa kuwa na huruma kwa wenzetu, jinsi tunavyoshindwa kuwasamehe wenzetu au jinsi ambavyo tunajikinaisha katika ubinafsi na kuacha kumwabudu Mungu na badala yake kujiabudu sisi wenyewe.

Maji atupatiayo Kristo ni upendo wa Mungu ambao unafunika utupu wetu au uwazi wetu wa maisha ya kiroho. Tunadhani tumesimama kumbe hapana, tunajiona tumekamilika kumbe tunakosa kilicho cha muhimu katika maisha yetu. Huyu ndiye Kristo, ufunuo mkamilifu wa upendo wa Mungu kwetu sisi wanadamu. Safari yetu ya toba katika kipindi hiki cha Kwaresima inapaswa kutufikisha katika kukiri ukuu wa Kristo. Muendelezo wa mazungumzo ya Kristo na mwanamke huyu Msamaria yanaifafanua vilivyo safari hiyo ambapo mwishoni anamtambua kuwa Yeye ndiye Kristo.

“Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda”. Hitimisho hili la Injili ni wito wa kuwa wamisionari kwa maisha yetu mapya yaliyojaa uzima wa kimungu. Kilele cha kipindi hiki cha toba ni sherehe ya Pasaka, tunapoadhimisha mateso, kifo na ufufuko wa Bwana. Safari yetu ya kiroho katika kipindi hiki cha toba ni budi kutufikisha katika ushuhuda huo wa kimaisha na kuwa sababu ya kuwavuta wengine kwa Mungu. Huo ni wajibu wetu wa kikristo ambao Kristo ametupatia kwenda kuwafundisha wote na watakaolipokea neno lake na kuliamini wataokoka (Rej Mk 16:15 – 16), yaani watakuwa na uzima wa kimungu.

Kristo anauchukua ubinadamu wetu kusudi kutufufunza umuhimu wa kujitoa na kuwa chanzo cha uhai kwa wengine. Mtume Paulo anatuambia kwamba “kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu”. Yeye analitekeleza lile alilolifanya Musa kwa ajili ya Waisraeli lakini sasa ni katika muktadha wa kiroho. Kwa kujitoa kwake sote tunarudishiwa uhai wetu kiroho ambao ulipotezwa na dhambi zetu. Ni wito kwetu sote tunapokuwa katika safari hii kumgeukia Mungu ili tupate uzima na kwa kuupata uzima huo tutakuwa sababu ya uhai kwa wengine.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.