2017-03-16 10:07:00

Bikira Maria wa Fatima: Ujumbe wa matumaini, toba na wongofu wa ndani


Mama Kanisa anaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea watoto wa Fatima yaani Francis, Yacinta na Lucia. “Papa Francisko mjini Fatima 2017 pamoja na Bikira Maria kama mahujaji wa matumaini na amani” ndiyo kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Ureno. Kimsingi, ujumbe wa Bikira Maria kwa watoto wa Fatima unafumbatwa katika matumaini, toba na wongofu wa ndani; mambo msingi yanayowawezesha waamini kutambua uwepo endelevu wa Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Familia na Parokia ni mahali ambapo waamini wanaweza kurithishana ujumbe wa Bikira Maria, ili Moyo Safi wa Bikira Maria uweze kuheshimiwa na kuthaminiwa!

Bikira Maria aliwatokea Watoto wa Fatima kunako mwaka 1917, wakati walimwengu walipokuwa wanateseka kutokana na Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na kuwapatia ujumbe wa matumaini uliokuwa unafumbatwa kwa namna ya pekee katika toba na wongofu wa ndani; sala na kwamba, Mwenyezi Mungu daima anatembea katika historia ya maisha ya watu wake, mwaliko kwa waamini kumtumainia Kristo Yesu kwani yeye ameushinda ulimwengu. Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali alipokuwa anachangia mada kuhusu ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima, kama sehemu ya maandalizi ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko huko Fatima nchini Ureno kuanzia tarehe 12- 13 Mei 2017. Anakiri kwamba, tangu akiwa bado kijana alipata kusikia kuhusu Bikira Maria kuwatokea watoto wa Fatima, akashuhudia mwenyewe dhamana na nafasi ya Bikira Maria katika maisha na utume wa Kanisa na kwa namna ya pekee kabisa alipomwona Mtakatifu Yohane Paulo II akijikabidhi kwa Bikira Maria “Totus tuus”.

Bikira Maria ameendelea kupewa kipaumbele cha pekee hata wakati wa uongozi wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na kwa sasa Papa Francisko ambaye kweli ameonesha ibada ya pekee kwa Bikira Maria anakwenda nchini Ureno kama hujaji wa matumaini na amani. Wanataalimungu wameendelea kuwasaidia waamini kutambua nafasi na dhamana ya Bikira Maria katika maisha na utume wa Kanisa. Lakini, ikumbukwe kwamba, Maandiko Matakatifu ni kiini cha ufunuo wa Mungu kwa waja wake pamoja na Mapokeo ya Kanisa. Lakini, Mwenyezi Mungu ameendelea kutenda maajabu kwa nyakati mbali mbali kwa njia ya Bikira Maria na watakatifu, ili kuwawezesha waamini kutambua mapenzi ya Mungu katika maisha yao, kazi ya Roho Mtakatifu.

Mama Kanisa anafundisha kwamba ingawa Ufunuo umekamilika, bado haujafafanuliwa kikamilifu. Ni juu ya imani ya Kikristo kuufahamu kwa taratibu jinsi ulivyo karne hadi karne. Huu ni msingi wa Ibada kwa Bikira Maria kwa watu wa nyakati zote. Ujumbe wa Bikira Maria wa Fatima ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani kwa Kristo na Kanisa lake, kwani Kristo Yesu alikuja duniani ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele! Askofu Antònio Dos Santos Marto wa Jimbo Katoliki Leiria-Fatima, Ureno anasema ujumbe wa Bikira Maria kwa watoto wa Fatima unafumbatwa kwa namna ya pekee katika neema na huruma ya Mungu inayoganga, kuponya na kusamehe majeraha ya mwanadamu! Huu ndio ujumbe wa matumaini unaobubujika kutoka katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima yaani: Francis, Yacinta na Lucia. Leo hii kuna majanga makubwa yanayoendelea kumwandama mwanadamu lakini upendo wa Mungu ni mkubwa sana kwa waja wake, changamoto kwa waamini ni kujiaminisha kwa Yesu ili aweze kuwapatia ulinzi na tunza yake kwa maombezi ya Bikira Maria, kwani daima yuko pamoja nao hadi utimilifu wa dahali!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.