2017-03-14 14:52:00

Askofu mkuu Luigi Barbarito amefariki dunia!


Askofu mkuu Angelo Becciu, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican, Jumanne, tarehe 14 Machi 2017 ameongoza mazishi ya Askofu mkuu Luigi Barbarito, Balozi mstaafu wa Vatican aliyefariki dunia usiku wa kuamkia tarehe 12 Machi 2017 huko Pietrafedus, Jimbo Katoliki la Avellino, nchini Italia. Askofu mkuu Barbarito alizaliwa kunako tarehe 19 Aprili 1922. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, kunako tarehe 20 Agosti 1944 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 11 Juni 1969 akateuliwa na Mwenyeheri Paulo VI kuwa Askofu mkuu na kuwekwa wakfu tarehe 10 Agosti 1969.

Tangu wakati huo alibahatika kutekeleza utume wake kama Balozi wa Vatican nchini Haiti, Senegal, Mali, Mauritania, Guinea Bissau, Australia na Uingereza. Anakumbukwa sana nchini Uingereza kwa kusaidia kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Uingereza na Vatican; Kati ya Kanisa Anglikani na Kanisa Katoliki. Hayati Askofu mkuu Luigi Barbarito alikuwa mahiri sana katika masuala ya kitaalimungu! Aliwahudumia na kuwapenda watu wa Mungu katika nchi hizi, kwa upendo ule unaobubujika kutoka kwa Mama Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya mtu mzima: kiroho na kimwili kama alivyokaza kusema, Mwenyeheri Paulo VI.

Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Becciu amewasilisha salam za rambi rambi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Kwa njia ya Ubatizo, Askofu mkuu Barbarito alizaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu na hivyo kushiriki katika Fumbo la Pasaka ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Katika maisha yake alibahatika kuwa mwakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro sehemu mbali mbali za dunia, utume alioufanya kwa weledi, juhudi, bidii, maarifa, imani na matumaini makubwa. Neno la Mungu, linawaalika waamini kutembea katika upya wa maisha kwa kufuata nyayo za Yesu katika wema, huruma na unyenyekevu. Marehemu Askofu mkuu Barbarito  alikuwa ni mkweli, mwema, mtu mwenye huruma na mkarimu.

Alibahatika kuwa na kipaji cha akili alichokitumia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo aliye njia, ukweli na uzima. Aliweza kukabiliana na changamoto za maisha kwa imani na matumaini makubwa, daima akilitanguliza Fumbo la Msalaba katika njia ya maisha yake. Alimtumainia na kujikabidhisha kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake, kwani ndiye aliyekuwa nguzo na usalama wa maisha yake. Familia ya Mungu inamponsikindikiza Askofu mkuu Luigi Barbarito katika usingizi wa amani, Kanisa litaendelea kumkumbuka kutokana na ushuhuda wake wa imani na matumaini na kwamba, alimtumainia sana Kristo katika maisha yake, bila shaka sasa ataweza kuuona Uso wake wenye huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.