2017-03-13 14:30:00

Papa Francisko: Jengeni utamaduni wa kusikiliza na kujadiliana!


Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Parokia ya Mtakatifu Magdalena wa Canossa, Jumapili, tarehe 12 machi 2017 alipata bahati ya kukutana na kuzungumza na watoto, wazazi na walezi wa watoto waliobatizwa katika kipindi cha mwaka uliopita, wazee pamoja na wagonjwa. Akizungumza na watoto wadogo, Baba Mtakatifu aliweza kuwajibu maswali yao. Amewaambia watoto hawa kwamba, Yesu anapenda kuwa karibu sana na waja wake wanapomwendea kwa moyo mnyofu, toba na wongofu wa ndani! Yesu daima yuko tayari kukutana na waja wake ili kuwaonjesha huruma, upendo na msamaha katika maisha yao.

Yesu daima yuko mioyoni mwao wakati wote wa maisha yao! Katika shida na magumu ya maisha, anawafariji. Baba Mtakatifu anasema, hakuna Chuo wala shule inayowaandaa Mapadre kuwa Makardinali wala Mapapa! Hakuna kutoa kitu kidogo ili kuchaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwani huu ni utume na dhamana ambayo mtu anakabidhiwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Petro ndiye aliyekuwa kiongozi mkuu wa kwanza wa Kanisa kuchaguliwa na Kristo Yesu, licha ya kumkana mara tatu, lakini bado aliweza kumwombea, kumsamehe na kumpokea jinsi alivyo kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anasema, katika maisha na utume wake, kama Padre, Askofu na sasa Khalifa wa Mtakatifu Petro amefurahia maisha na utume wake. Alipenda sana kufundisha katekesi kwa watoto wadogo, kuadhimisha Ibada ya Misa kwa watoto; daima ameridhika kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake! Kwa utume wake, ameteuliwa kuwa ni chombo cha haki, amani, upendo na mshikamano; tunu msingi za maisha ya Kikristo zinazopaswa kumwilishwa katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu.

Wazazi wanapaswa kujifunza kujipatanisha daima na kamwe wasikubali hasira iwatale katika mioyo yao; wawe daima ni mashuhuda wa upatanisho. Watoto wajifunze kuwa wema na watakatifu na kamwe wasiwatukane watu wala kukufuru. Jambo linalomwogofya zaidi katika maisha anasema Baba Mtakatifu ni ubaya wa watu unaojikita katika mioyo yao, matokeo ya dhambi asili. Anasikitishwa sana na uzushi na maseng’enyo dhidi ya watu wengine, ni afadhali maradufu kwa mtu anayetupa bomu na kutokomea mbali kuliko watu wanaowaseng’enya wenzao na kupandikiza mbegu ya fitina na chuki, ni hatari kwani haya ni mambo yanayoharibu maisha ya watu iwe ndani ya familia, jamii na hata Vatican kwenyewe huko!

Watu wa namna hii wanaweza kuitwa pia ni “magaidi” kwani wanataka kuteketeza maisha ya wengine. Watu wajifunze kutenda mema na kuachana na ubaya. Nyakati nzuri zaidi katika maisha yake anasema Baba Mtakatifu Francisko ni wakati alipokuwa mtoto mdogo alipenda kuandamana na wazazi wake kwenye Uwanja wa michezo kuangalia mpira; alipenda kukutana na kucheza na marafiki zake; anapopata nafasi ya kusali katika kimya kikuu; kwa kusali na kulitafakari Neno la Mungu. Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa wema na ukarimu katika maisha yake. Hata watoto hawa wamemhakikishia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, kati ya siku nzuri walizobahatika kuwa nazo katika maisha yao ni kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro, hasa Jumapili ya terehe 12 Machi 2017 wakati anapojiandaa kuadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 4 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki.

Baba Mtakatifu amewapongeza Makatekista wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa; wako mstari wa mbele katika kufundisha Katekesi pamoja na kutekeleza matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika Parokia na Majimbo yao. Makatekista wanayo dhamana ya kufundisha: Imani ya Kanisa, Sakramenti, Amri za Mungu na Sala; hii ni dhamana nyeti sana! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya kijamii inayowawezesha watu wengi kuwasiliana! Lakini kwa bahati mbaya, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kimekuwa ni chanzo kikuu cha kusambaratika kwa mawasiliano katika familia na jamii katika ujumla wake. Badala ya kukuza na kudumisha majadiliano matokeo yake, hakuna tena utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana, watu wamezama sana katika matumizi ya teknolojia ya habari kiasi hata cha kushindwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu!

Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana katika ukweli na uwazi; kwa kuhudumiana katika huruma na upendo. Majadiliano ni daraja la watu kukutana. Amewashukuru wazazi na walezi wa watoto waliobatizwa mwaka uliopita na kuwataka wawasaidie watoto wao kukua katika imani na kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu ameahidi kuendelea kusali kwa ajili ya wagonjwa na wazee na kwamba, ugonjwa ni Msalaba na mbegu ya maisha mapya. Amewaomba kumsindikiza katika maisha na utume wake ili aendelee kuwa Padre, mwema, mnyofu na mtakatifu. Mwishoni kabisa, Baba Mtakatifu amewashukuru wanaparokia ya Mtakatifu Magdalena wa Canossa kwa ukarimu na upendo waliomwonesha na kuwataka kusonga mbele kwa imani, matumaini na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.