2017-03-13 14:00:00

Kwaresima iwasaidie waamini kutafakari Fumbo la Msalaba na Dhambi


Tukio la kung’ara kwa Yesu mbele ya Mitume wake kadiri ya Mwinjili Mathayo linaonesha: Ukuu, utakatifu, uzuri, furaha na chemchemi ya maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Hii ni siri ambayo walitakiwa kuizamisha katika sakafu ya mioyo yao mpaka baada ya mateso, kifo na ufufuko wake. Hii ina maanisha kwamba, baada ya Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko, Yesu atakuwa na Uso tofauti kabisa, uso ambao utakuwa umechubuliwa kwa taji la miiba kichwani; uso unaotokwa damu; uso ambao umeonja mateso na machungu makubwa! Hiki ndicho kielelezo cha Fumbo la Msalaba linalofafanuliwa na Yesu mbele ya wafuasi wake katika tukio hili la kung’ara uso, Jumapili ya pili ya Kipindi cha Kwaresima.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni, tarehe 12 Machi 2017 alipotembelea Parokia ya Mtakatifu Magdalena wa Canossa, nje kidogo ya Jimbo kuu la Roma ili kusali na kuzungumza na familia ya Mungu eneo hili. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuutafakari Msalaba ambao juu yake alitundikwa Yesu Mwana wa Mungu; ambaye wanaalikwa kumsikiliza kwa makini. Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake amejinyenyekesha hata kufa Msalabani. Mtakatifu Paulo anasema, “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye”.

Dhambi inaharibu uhusiano mwema kati ya Mungu na mwanadamu; dhambi inakwenda kinyume cha mapenzi ya Mungu na kwamba dhambi inamfanya mwanadamu  kushindwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa Mwenyezi Mungu. Lakini, Yesu alijinyenyekesha sana kiasi cha kukubali kusulubiwa juu ya Msalaba ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Tukio la kung’ara Bwana anasema Baba Mtakatifu ilikuwa ni sehemu ya mbinu mkakati wa Yesu kuwaandaa wafuasi wake ili kuweza kukabiliana na Kashfa ya Msalaba.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, waamini ni wepesi sana kuzungumzia kuhusu dhambi na hasa pale wanapokimbilia kwenye Sakramenti ya huruma ya Mungu, wanajisikia kwamba, kweli wamesamehewa na Mwenyezi Mungu, kwani Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake amezibeba dhambi za binadamu. Waamini wanahamasishwa kuwa na ujasiri wa kuzifahamu, kuziungama, kuzitubu na kukusudia kuziacha dhambi, ili kupata msamaha na maondoleo ya dhambi kutoka kwa Kristo Yesu, kama sehemu ya mchakato wa safari ya kuelekea kwenye maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Yesu, ili kushiriki mwanga wa maisha yake ya uzima wa milele.

Kwa njia ya Msalaba, Yesu amelipa deni la dhambi za binadamu, akawa ni kashfa mbele ya Mungu; Mwana Mpendwa wa Mungu katika mateso yake, akaonekana kulaaniwa kwa vile alijitwika dhambi za binadamu! Mtakatifu Paulo anasema “Kristo alitukomboa katika laana ya Torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu, kwani imeandikwa, kila mtu aangikwaye juu ya mti, ili kwamba, baraka ya Ibrahim iwafikie Mataifa katika Yesu Kristo, ili tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani” (Rej. Gala. 3: 10- 14). Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani, mwaliko kwa kuwa na ujasiri ili kuutafuta Uso wa Yesu ili kuweza kukutana naye katika maisha ya uzima wa milele.

Wakristo wasonge mbele katika njia inayowapeleka kwenye uzima wa milele na maisha ya Kikristo; kwa kuomba msamaha wa dhambi na kukusudia kuachana na dhambi pamoja na nafasi zake sanjari na kuwa na imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu ambaye kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake amejitwalia dhambi za binadamu! Waamini wawe na ujasiri wa kufanya toba na kuomba msamaha wa dhambi zao anasema Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya hatima ya mahubiri yake kwenye Parokia ya Mtakatifu Magdalena wa Canossa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.