2017-03-10 12:19:00

Papa na wasaidizi wake wachanga Euro 100, 000 kwenda Aleppo, Syria


Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi waandamizi kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican, maarufu kama “Curia Roma” wamehitimisha mafungo ya Kwaresima yaliyoanza tarehe 5  hadi tarehe10 Machi 2017 huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma. Mafungo haya yameongozwa na Padre Giulio Michelini. Tema iliyochaguliwa ni “Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kadiri ya Injili ilivyoandikwa na Mtakatifu Mathayo.”

Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni mwa mafungo haya, Ijumaa asubuhi tarehe 10 Machi 2017 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutolea nia kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Syria. Baba Mtakatifu ametoa kiasi cha Euro 100, 000 kwa ajili ya kuwasaidia maskini walioko mjini Aleppo. Haya ni majitoleo ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na waandamizi wake waliokuwa wanashiriki kwenye mafungo ya kiroho huko Ariccia. Msaada huu utapelekwa moja kwa moja kwa walengwa kupitia kwa mtunza sadaka mkuu wa Papa kwa kushirikiana na Mtunza Maeneo Matakatifu katika Nchi Takatifu.

Haya yamebainishwa na Dr. Paloma García Ovejero, Msemaji msaidizi wa Vatican ambaye amefafanua pia kwamba, Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi waandamizi kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican wamerejea mjini Vatican majira ya saa 5:30 asubuhi kwa saa za Ulaya. Jioni Baba Mtakatifu anakutana na Maparoko wakuu kwenye Makao makuu ya Jimbo kuu la Roma. Mkutano huu utakuwa ani wafaragha na ni sehemu shughuli zake za kawaida kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.