2017-03-10 09:30:00

Nafasi na dhamana ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa


Padre Raniero Cantalamessa mhubiri wa nyumba ya kipapa anasema, kauli mbiu inayoongoza tafakari za kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2017 ni “Hawezi mtu kusema Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu”. (Rej. 1 Kor. 12: 3) Imani kwa Kristo Yesu inawezekana tu kwa njia ya Roho Mtakatifu na kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Mkristo anashirikishwa kwa karibu sana Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ndiyo maana mahubiri ya Kwaresima kwa mwaka 2017 yanajikita zaidi katika Roho Mtakatifu “anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana” Roho Mtakatifu ni sehemu ya mpango mzima wa Mungu katika ukombozi wa mwanadamu.

Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, vyombo vya habari ndivyo vinavyotoa vipaumbele vya kushughulikiwa na mwanadamu katika ustawi na maendeleo yake. Kwa Kanisa, Roho Mtakatifu ndiye mleta uzima, atokaye kwa Baba na Mwana. Padre Cantalamessa anakaza kusema, tema ya tafakari za kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2017 ni mwendelezo wa tema zilizofanyiwa tafakari wakati wa Kipindi cha Majilio. Lengo ni kumtafakari Roho Mtakatifu, Nafsi ya tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na shughuli zake katika historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu!

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walitoa dira na mwelekeo mpya katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa Roho Mtakatifu anayeishi na kutenda kazi ndani ya Kanisa la Kristo. Mwaka 2017, Chama cha Kitume cha Uhamsho wa Kikatoliki kinaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Hiki ni chama ambacho kimewagusa na kuwaunganisha mamilioni ya Wakatoliki sehemu mbali mbali za dunia. Nia ya Baba Mtakatifu Francisko ni kuona kwamba, Jubilei inasherehekewa Kiekumene kwa namna ya pekee wakati wa Siku kuu ya Pentekoste kwa mwaka 2017 ambayo itaadhimishwa hapo tarehe 4 Juni 2017.

Padre Cantalamessa anakaza kusema, tafakari zake zinapenda kuonesha nafasi na dhamana ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa; maana ya maisha na hatima ya maisha ya binadamu mintarafu Fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Roho Mtakatifu ndiye anayezima kiu cha maswali na udadisi wa binadamu kutoka katika undani wa maisha yake. Roho Mtakatifu anawasaidia waamini kuufahamu ukweli wote yaani: Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kiini cha imani ya Kanisa. Hii ni changamoto kwa waamini kutambua nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha, ili kuweza kumpatia kipaumbele cha kwanza. Roho Mtakatifu ni nguzo thabiti kwa wale wanaomwamini na kumtumaini katika maisha yao.

Padre Cantalamessa katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano anasema, Roho Mtakatifu yuko daima katika maisha na utume wa Kanisa kama  Nafsi ya Tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ndiye anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana. Roho Mtakatifu ni mfariji na wakili; ni Roho wa Kristo, Roho wa Bwana anayetambulika kama: Maji, Mpako, Moto, Wingu na nuru, Muhuri wa Baba wa milele, Mkono na kwamba, Roho Mtakatifu ni kidole cha Mungu na hua, alama ya amani, utulivu na utakaso. Waamini wanapewa changamoto na Mama Kanisa ya kumwalika daima Roho Mtakatifu katika maisha yao ya kila siku, ili awasaidie katika kufikiri, kutenda na kupenda zaidi. Roho Mtakatifu ni chemchemi ya upendo halisi anayeweza kunyeeshea pakavu pa maisha ya mwanadamu!

  1. Uje Roho Mtakatifu tuangaze toka mbingu, Roho zetu kwa mwangao, Ewe Mungu Roho njoo.
  2. Uje Baba wa maskini, uje mtoa wa vipaji, uje mwanga wa mioyo, Ewe Mungu Roho njoo.
  3. Ee Mfariji mwema sana, ee rafiki mwanana, ee raha mustarehe, Ewe Mungu Roho njoo.
  4. Kwenye kazi u pumziko, kwenye joto burudisho, u mfutaji wa machozi, Ewe Mungu Roho njoo.
  5. Ewe mwanga wenye heri, uwajaze waamini, neema yako mioyoni, Ewe Mungu Roho njoo.
  6. Bila nguvu yako wewe, mwanadamu hana kitu, kwake yote yana kosa, Ewe Mungu Roho njoo.
  7. Osha machafuko yetu, panyeshee pakavu petu, na kuponya majeraha, Ewe Mungu Roho njoo.
  8. Ulegeze ukaidi, pasha moto ubaridi, nyoosha upotevuu wetu, Ewe Mungu Roho njoo.
  9. Wape waamini wako, wenye tumaini kwako, paji zako zote saba, Ewe Mungu Roho njoo.
  10. Wape tuzo ya fadhila, wape mwisho bila ila, wape heri ya milele, Ewe Mungu Roho njoo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.