2017-03-09 15:00:00

Mahojiano na Papa: Hija za kitume, changamoto ya miito, imani na utume


Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alifanya mahojiano maalum na Gazeti la “Die Zeit” kutoka Ujerumani ambamo anagusia pamoja na mambo mengine, ziara zake za kichungaji kwa siku za usoni, matangazo yaliyosambazwa mjini Roma kupinga mageuzi yanayofanywa kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican, mtikisiko uliolikumba Shirika la Kijeshi la Malta kiasi cha kumfanya kiongozi wake mkuu kuwajibika kimaadili. Katika mahojiano haya, Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, yeye ni mtu wa kawaida, anajitambua kuwa ni mdhambi, mwenye karama na mapungufu yake kama binadamu! Anajitahidi kufikiri na kutenda kadiri ya uwezo wake.

Kwa wale wanaotarajia mambo makubwa kutoka kwake anasema, wanamkosea haki! Yeye ni mtu wa kawaida na kwamba, anatambua kuwa kuna baadhi hawaridhiki na jinsi anavyofikiri na kutenda. Anasema, kumekuwepo na mashambulizi makali yanayoelekezwa dhidi ya Vatican, lakini tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa, daima ameendelea kuwa ni mtu mwenye furaha na amani ya ndani. Kuna njia mbali mbali za kufikiri na kutenda ni jambo la kawaida katika maisha ya mwanadamu na kwamba, huu ni utajiri mkubwa unaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa!

Baba Mtakatifu anasema matangazo yaliyobandikwa hivi karibuni kwenye viunga vya Jiji la Roma kwa kumkashifu kwamba, si kiongozi anayeshuhudia huruma, hili ni jambo la kuchekesha sana anasema Baba Mtakatifu Francisko. Hii inatokana na ukweli kwamba, mtu aliyeandika matangazo haya anazo sababu zake msingi, kumbe, hawezi kukosa amani na furaha moyoni kwani furaha hii inarutubishwa kwa namna ya pekee na sala ya Mtakatifu Thomas More, ambaye alikuwa anamwomba Mwenyezi Mungu amjalie kipaji cha ucheshi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Shirika la Kijeshi la Malta hivi karibuni lilikumbwa na mtikisiko wa kimaadili katika utendaji wake, kiasi cha Kardinali Raymond Leo Burke kushindwa kumudu hali hiyo! Kutokana na umuhimu wa Shirika hili katika kulinda na kushuhudia imani sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya huduma makini, kama Khalifa wa Mtakatifu Petro aliamua kuingilia kati ili kuwarejeshea tena watu imani na matumaini kwa chombo hiki muhimu sana katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anasema, Kardinali Raymond Burke hakuwa peke yake katika mgogoro huu, ndiyo maana ameamua kumteua Askofu mkuu Angelo Becciu kusimamia mchakato mzima wa upyaisho na majiundo ya maisha ya kiroho na kimaadili ya Shirika la Malta. Baba Mtakatifu anasema, Kardinali Raymond Burke ataendelea kuwa ni Msimamizi mkuu wa Shirika la Kijeshi la Malta.

Baba Mtakatifu Francisko akijibu swali kuhusu uhaba wa miito mitakatifu ndani ya Kanisa anasikitika kusema kwamba, hili ni tatizo na changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ikumbukwe kwamba, Mapadre ni mashuhuda na vyombo vya Sakramenti za huruma ya Mungu; mahali ambapo hakuna Padre hakuna Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Upatanisho na Mpako wa wagonjwa! Hizi ni Sakramenti zinazotolewa na Mapadre peke yao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu. Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu ni nyenzo msingi katika ujenzi wa Kanisa, kwani Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa! Mahali ambapo hakuna adhimisho la Ekaristi Takatifu, hapo hakuna Kanisa. Ukosefu wa mapadre ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Kuna mambo mengine yanayochangia katika hali hii, kwanza kabisa ni idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa; hali ngumu ya uchumi; ukosefu wa fursa za ajira pamoja na ukosefu wa vijana wenye nia na shauku ya kutaka kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Hata hivyo, Kanisa halina budi kuwa makini katika mchakato wa kuwachagua vijana wanaotaka kumtumikia Mungu na jirani zao kwa njia ya Daraja Takatifu! Hawa ni vijana wanaopaswa kuteuliwa, kuandaliwa na kusindikizwa vizuri ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, vinginevyo anasema Baba Mtakatifu, vijana hawa watakuwa ni mzigo mkubwa kwa familia ya Mungu watakayokuwa wanaiongoza! Hakuna haja ya kuwa na wongofu wa shuruti, jambo la msingi kwanza ni vijana kupata fursa za kazi ili kujenga matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu anasema useja ni zawadi kubwa kwa Kanisa, licha ya magumu na changamoto zake! Kumbe, kuna haja ya wakleri kujiaminisha mbele ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasema katika hija ya maisha ya kiroho kuna nyakati za giza kiasi cha mwamini kushindwa kuona mwanga; kuna nyakati za majaribu kiasi hata cha mwamini kukata tamaa ya maisha; yote haya ni matokeo ya dhambi ya asili, kiasi cha kumfanya mwamini kumkasirikia Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anakiri kwa kusema kwamba, hata yeye katika maisha, amepitia nyakati kama hizi. Lakini, daima Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo kwa wadhambi wanaotubu na kumwendea kwa moyo uliovunjika na kupondeka!

Majaribu ya maisha yakichukuliwa kwa moyo wa imani na matumaini ni chachu ya ukomavu wa imani, matumaini na mapendo. Yote haya ni sehemu ya mapito ya mwanadamu, vinginevyo mwamini atashindwa kupata ukomavu katika maisha yake na kubaki kuwa ni mtoto! Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake, alianguka na kupoteza imani na matumaini, lakini kwa msaada wa Kristo Yesu aliweza kusimama tena na kusonga mbele, kiasi hata cha kukabidhiwa dhamana ya kuliongoza Kanisa.

Ikumbukwe kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayorutubishwa kwa tafakari, maisha ya Sakramenti na kumwilishwa katika matendo ya huruma! Waamini wanapaswa kuondokana na woga pamoja na wasi wasi usiokuwa na mashiko wala mvuto kwani, haya ni mambo yanayomfungia mwamini mlango wa matumaini. Jambo la msingi ni kwa waamini wenyewe kuwa huru na wajasiri, kiasi cha kuthubutu kumfungulia Mungu malango ya maisha yao.

Binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kimsingi, mwanadamu ni mwema, lakini amejeruhiwa, kumbe ni mnyonge, hali kama ilivyojitokeza kwa Adamu; Kaini akaonesha ukatili dhidi ya ndugu yake Abeli. Ni mtu aliyetawaliwa na chuki, uhasama na wivu uliofunika utashi wake kiasi cha kutumbukia katika maovu haya makubwa. Ukatili huu unajionesha hata katika vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; wafanyabiashara wanatengeneza na kusambaza silaha zinazoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Hata Kanisa linapaswa kuonesha uaminifu na ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Injili ya Kristo kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya!

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, kuna wanasiasa wanaojitafutia umaarufu ili kujijenga kiasiasa, lakini ni watu hatari katika maisha ya kijamii. Wanasiasa mashuhuri baada ya kuona madhara ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia wakajipanga na kuamua kuanzisha Umoja wa Ulaya, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu; upendo na mshikamano; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hawa ni watu ambao hawakupenda kujitwalia ujiko, kwani wale wote wanaotafuta madaraka kwa nguvu, mara nyingi ni watu wanaoishia pabaya kama historia inavyowafundisha walimwengu.

Leo hii dunia inaendelea kuathirika kutokana na Vita Kuu ya Tatu ya Dunia inayopiganwa vipande vipande sehemu mbali mbali za dunia! Kuna watu wanaendelea kupoteza maisha Barani Afrika, Asia, Ukraine na huko Mashariki ya Kati hasa Iraq. Watu wanapigana vita kwa kutumia silaha za kisasa kabisa ambazo zinasababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao. Hii ni kazi kubwa inayofanywa na viwanda vya kutengeneza silaha duniani.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwenye ratiba yake elekezi kwa Mwaka 2017 anatarajia kutembela Indian a Bangaladesh; Colombia na Fatima. Kuna mpango wa hija ya kiekumene Sudan ya Kusini, ili kushuhudia mateso na mahangaiko ya familia ya Mungu nchini humo kutokana na vita na baa la njaa, lakini bado kuna mashaka ikiwa kama safari hii inaweza kutekelezeka. Kulikuwepo na mpango wa kutembelea DRC na Congo Brazzaville, lakini kwa sasa hali ya kisiasa bado ni tete sana. Vatican ilikuwa iangaalia uwezekano wa kutembelea Russian a Ukaraine. Hizi ni kati ya safari ambazo anatarajia kuzifanya, sehemu mbali mbali za dunia, Mwenyezi Mungu akipenda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.