2017-03-08 13:39:00

Yanayojiri katika mafungo huko Jangwani alikojichimbia Papa Francisko


Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya habari na hasa matumizi makubwa ya simu za mkononi yanaonekana kufifisha sana mahusiano mubashara kati ya watu na hasa zaidi ndani ya familia. Simu za mkononi pamoja na faida zake kubwa lakini pia zimekuwa ni chanzo cha majanga makubwa katika maisha ya ndoa na familia. Chakula cha pamoja kadiri ya Mapokeo ya Kikristo ni alama ya upendo, mshikamano na sehemu ya kumbu kumbu ya wokovu. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Padre Giulio Michelini, Jumanne, tarehe 7 Machi 2017 mbele ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na waandamizi wake kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican ambao kwa sasa wamejichimbia “Jangwani” kwa ajili ya tafakari ya Kwaresima kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Tafakari hii inaongozwa na kauli mbiu “Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kadiri ya Injili ilivyoandikwa na Mtakatifu Mathayo.” Kiini cha tafakari ya siku kilikuwa ni sehemu ya Injili ya Mathayo 26: 20- 35: Mkate na Mwili wa Yesu; Divai na Damu Azizi ya Yesu.

Padre Michelini amewataka wafungaji wake kugundua tena ule uzuri na utakatifu wa kukaa pamoja kwa chakula ili kudumisha upendo na mshikamano na hivyo kuondokana na ile chachu ya usaliti iliyooneshwa na Yuda Iskariote wakati wa Karamu ya Mwisho, iliyopaswa kuwa ni kielelezo cha huduma, upendo na mshikamano wa dhati! Kuna hatari kwa wakleri kutekeleza dhamana na wajibu wao kama watu wa mshahara bila kuzingatia amri ya upendo kwa Mungu na jirani; haki inayomwilishwa katika huruma ya Mungu, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Padre Michelini amewataka wakleri kutafakari tena na tena Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anamo bainisha umuhimu wa kutumia vyema rasilimali ya dunia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Amekazia ukarimu, upendo na mshikamano kwa kuhakikisha kwamba, chakula kinatumiwa vyema. Watu wawe makini kwa ubora na wingi wa chakula wanachopata sanjari na kupata muda mzuri wa kula chakula hicho ili kiweze kuleta mafao na ustawi kwa maisha ya mwanadamu.

Chakula kiwe ni mahali pa kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, ili kuondokana na kashfa iliyojitokeza kwenye Jumuiya ya Wakristo wa Korintho waliokuwa wanalalamikiwa na Mtakatifu Paulo kutokana na chakula kuwa ni chanzo cha kinzani na migawanyiko miongoni mwa Wakristo! Hii ni changamoto ambayo pia inapaswa kufanyiwa kazi katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili kweli adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu liweze kuwa ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Bado kuna safari ndefu kwa Wakristo kufikia muafaka wa kuadhimisha Ekaristi Takatifu kwa umoja!

Padre Michelini katika tafakari yake ya tatu amejikita zaidi kuhusu “Msamaha wa dhambi” uliotekelezwa kwa dhati kwa njia ya mateso na kifo cha Kristo Yesu, aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni kwa njia ya Damu yake azizi, mwanadamu amepata msamaha wa dhambi!. Padre Michelini amefafanua kwa kina na mapana maneno ya Yesu wakati alipokuwa anaweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kumbu kumbu endelevu ya uwepo wake, msamaha na huduma.

Katika Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 26: 1- 19: Yesu anaanza kugusia kuhusu Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko wake! Ni mwanzo wa mapambano ya kukubali kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake, kiasi cha kujiachilia mikononi mwa Baba yake wa Mbinguni pale juu Msalabani aliposikika akilia kwa sauti “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu”. Mwinjili Luka na Yohane hawakutaka kuweka kilio cha Yesu Msalabani katika Injili zao, lakini kazi hii imefanywa kwa ufundi mkubwa na Mwinjili Mathayo!

Padre Michelini anakaza kusema, Yesu alitumia: Mkate na Divai kuwa ni kielelezo cha Mwili na Damu yake Azizi; Alitumia kimya kikuu pale juu Msalabani, kama kielelezo cha sala, upendo na huruma kwa binadamu; sala ambayo ilikuwa inapaa mbinguni kama uvumba. Ukimya wa Yesu unaweza kufafanuliwa kwamba huo ulikuwa ni utulivu wa ndani, kiasi cha kusababisha wasi wasi na hofu kwa wale waliomzunguka. Yesu alijiandalia Pasaka yake kwa utulivu na hakutaka kuharibu Siku kuu ya Pasaka ya Wayahudi waliokuwa tayari wanataka kumwondoshea mbali utadhani alikuwa ni “gaidi wa kutupwa”.

Yale mafuta ya marhamu safi aliyopakwa Yesu, yakaonekana kuwa ni uharibifu wa mali ambayo ingeweza kutumika kuwasaidia maskini. Marhamu safi ni utakatifu wa maisha ya Yesu unaolijaza Kanisa lake! Inasikitisha kuona kwamba, majitoleo ya yule mwanamke asiyekuwa na jina, yanapigwa “madongo” kwa vile tu ametendewa Yesu na kusahau kwamba, Yesu mwenyewe alijisadaka kiasi kwamba, hakuwa na chochote cha kujivunia. Yesu anamtetea mwanamke wa Bethania, ili kuwapatia nafasi maskini kushiriki katika Karamu ya Pasaka.

Hii ni changamoto kwa waamini kuangalia ni jinsi gani ambavyo wanatangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake! Imani inatangazwa kwa njia ya maneno, matendo, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa watu! Uinjilishaji pia unafanyika kwa njia ya Ukimya; huduma makini kwa maskini, ili kuwainua katika maisha na utu wao na wala si kama wale wakuu wa makuhani waliopanga kumwangamiza Yesu. Liturujia na Sala za wakleri zilimwilishwe katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Anakaza kusema Padre Giulio Michelini wakati wa tafakari yake kwenye mafungo kwa Baba Mtakatifu Francisko na waandamizi wake kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican, maarufu kama “Curia Romana”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.