2017-03-06 13:25:00

UN inapania kudumisha haki msingi za binadamu duniani!


Bwana Zeid Raad Al Hussein, Kamishna mkuu wa Haki za Binadamu, Umoja wa Mataifa, hivi karibuni amezindua mpango mkakati unaotarajiwa kugharimu kiasi cha dola za kimarekani bilioni 253 ili kujizatiti zaidi katika kudumisha haki msingi za binadamu, sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni mradi wa aina yake kuwahi kuzinduliwa katika historia ya Umoja wa Mataifa. Hii inatokana na ukweli kwamba, kumekuwepo na uvunjwaji mkubwa wa haki msingi za binadamu, kwani watu wanavunja sheria kwa makusudi kabisa, kumekuwepo na vitendo vya unyanyasaji na ubaguzi mintarafu dini na rangi na mahali wanapotoka watu, mambo yanayovunja haki msingi za binadamu!

Bwana Zeid Raad Al Hussein anasema, hadi sasa, Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa kudhibiti vita, kinzani na mipasuko ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia, kiasi kwamba, kumekuwepo na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuzikimbia nchi zao, ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Umoja wa Mataifa, kwa kuhakikisha kwamba, Ofisi za Haki Msingi za Binadamu zinazoendeshwa na Umoja wa Mataifa katika nchi zaidi ya 70 zinafanya kazi barabara, ili haki msingi za binadamu ziweze kuheshimiwa katika ngazi ya kitaifa na kimataifa, kwa kuhakikisha kwamba, haki hizi zinapewa kipaumbele cha kwanza katika maisha ya watu na sera za nchi husika.

Bwana Zeid Raad Al Hussein anasikitika kusema kwamba, ukata wa rasilimali fedha, umezifanya ofisi za Haki Msingi za Binadamu za Umoja wa Mataifa kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake. Kumbe, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, sekta binafsi na mashirika ya kimataifa na kitaifa yanahamasishwa ili kuchangia katika utekelezaji wa mkakati huu, ili kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, sehemu mbali mbali za dunia. Fedha hii itasaidia kutekeleza mpango mkakati utakaoratibu masuala ya vita na mateso duniani pamoja na msaada katika maeneo ya vita ambayo hayafikiki kwa urahisi sana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.