2017-03-06 08:48:00

Kumbu kumbu ya miaka 40 ya uhusiano wa Kidiplomasia Ghana na Vatican


Familia ya Mungu nchini Ghana inaendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 40 ya uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican sanjari na miaka 60 tangu Ghana ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Mwingireza. Imekuwa ni fursa nyingine tena kwa familia ya Mungu nchini Ghana kujiweka wakfu chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu! Changamoto kwa waamini ni kukimbilia daima katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, kwa toba, wongofu wa ndani na matendo ya huruma kwa jirani zao, kielelezo makini cha huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake!

Askofu mkuu Jean-Marie Speich anasema, Ghana na Vatican ziliweza kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia, wakati hali ilikuwa tete sana nchini Ghana. Lakini, Mwenyeheri Paulo VI alipiga moyo konde akafanya maamuzi ya kinabii, leo hii familia ya Mungu nchini Ghana inaendelea kufurahia na kufaidika na matunda ya mahusiano kati ya pande hizi mbili. Kardinali Giuseppe Bertello amemwakilisha Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Bertello aliwahi kuwa Balozi wa Vatican nchini Ghana kati ya mwaka 1987 hadi mwaka 1991. Tukio hili, hapo tarehe 3 Machi 2017 limehudhuriwa na viongozi wa Serikali, Kanisa na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi na mashirika ya kimataifa nchini Ghana. Kulikuwepo wawakilishi kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, ambayo ina makao yake makuu nchini Ghana.

Askofu mkuu Jean-Marie Speich amefanya rejea ya historia ya uhusiano kati ya Vatican na Ghana katika kipindi cha miaka 40 iliyopita. Kwa namna ya pekee, amegusia mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Ghana hususan katika huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo endelevu ya watu. Leo hii, Kanisa Katoliki nchini Ghana lina miliki na kuendesha shule 4600 zinazohudhuriwa na asilimia 20% ya wanafunzi Wakatoliki na idadi kubwa ni waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo nchini Ghana. Kanisa linamiliki na kuendesha asilimia 27% ya miundo mbinu yote ya huduma ya afya nchini humo.

Tangu wakati huo anasema Askofu mkuu Jean-Marie Speich, utu na heshima ya wananchi wa Ghana vimepewa kipaumbele cha kwanza sanjari na mshikamano, umoja, ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Ghana, kiasi kwamba, Ghana ikawa ni mfano bora wa kuigwa na nchi nyingine za Kiafrika. Vatican inapenda kuendeleza ushirikiano na Ghana hasa katika huduma makini na endelevu zinazotolewa na Baraza la Kipapa la huduma endelevu za binadamu ambalo kwa sasa liko chini ya Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson kutoka Ghana. Katika kipindi chote hiki, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani, maridhiano na umoja wa kitaifa. Kardinali Giuseppe Bertello, tarehe 4 Machi 2017 aliongoza Masifu ya Jioni na kuiweka wakfu familia ya Mungu nchini Ghana chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Tarehe 6 Machi ni kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Ghana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.