2017-03-04 08:39:00

Ukarimu kwa Injili, Jimbo Katoliki Geita


Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita, Tanzania, katika barua yake ya kichungaji anapenda kuchukua nafasi hii kuialika familia ya Mungu Jimboni Geita kushuhudia ukarimu wao kwa Injili, ili kuweza kujibu kwa uhakika, changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo mintarafu maendeleo ya kina na ya jumla ya binadamu. Anawajulisha kuhusu azimio la ujenzi wa Hospitali na shule ya Sekondari ya Jimbo Katoliki Geita unaanza rasmi.

Huu ni ujenzi utakaofanywa na waamini wa Jimbo la Geita kama sehemu ya ukarimu wa kila binadamu muhitaji katika mazingira mbali mbali. Huu ni mwaliko pia kwa watu wote wenye mapenzi mema kuguswa na kusikiliza kilio cha maskini, tayari kukipatia majibu kwa mwanga wa Injili! Changamoto hii inaongozwa na kauli mbiu “Elimu na afya, nguvu yetu ya Uinjilishaji Geita”. Kwa hakika, huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ambamo, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuwa na chapa ya kudumu katika utekelezaji wa Injili ya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika huduma makini na matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha imani tendaji!

Hii itakuwa ni Hospitali ya Mtakatifu Yohane Paulo II na Shule ya Sekondari ya Yohane Paulo, Papa wa kwanza katika historia ya Kanisa kutembelea Tanzania na kuwakutanisha waamini wanaounda Jimbo kuu la Mwanza, kilimani Kawekamo, Jimbo kuu la Mwanza kunako mwaka 1990. Papa Yohane Paulo II akabariki Jiwe la Msingi la Kanisa kuu Jimbo Katoliki la Geita; akabariki pia Jiwe la Msingi la Seminari ya Bikira Maria Malkia wa Mitume, Sengerema. Askofu mkuu Damiani Dallu, wakati huo akiwa Askofu wa Jimbo la Geita, kwa kusoma alama za nyakati akaazimia kujenga shule ya Sekondari, ikiwa na Kituo cha huduma ya Afya kwa wanafunzi, kama heshima kwa Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili aliyejisadaka na kuonesha upendo mkubwa kwa vijana wa kizazi kipya! Askofu Flavian Kassala, katika barua yake kwa familia ya Mungu anataka kuendeleza mchakato wa kumuenzi Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kuwekeza katika ustawi na maendeleo ya vijana wa kizazi kipya katika elimu na afya!

Jimbo Katoliki la Geita linapenda kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yohane Paulo II linapoanza utekelezaji wa ndoto hii kubwa, ili kweli Mtakatifu Yohane Paulo II aendelee kuwa ni chachu ya ukarimu kwa familia ya Mungu Jimboni Geita; ukarimu ambao umeendelea kuwa ni chachu na siri ya mafanikio makubwa Jimboni Geita. Ukarimu wa Kiinjili anasema Askofu Flaviani Matindi Kassala kwamba, ni sehemu ya vinasaba vya familia ya Mungu Jimboni Geita. Katika kipindi cha mwaka mzima, mwamini atachangia kiasi cha shilingi elfu 24, 000 sawa na kiasi cha shilingi elfu 2,000 kwa kila mwezi.

Lengo ni kumpatia kila mwamini kuweka historia ya ukarimu wake ambao utakuwa ni chapa ya kudumu hata kwa vizazi vijavyo. Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele katika Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa limewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu ya binadamu, ili kumletea ukombozi wa kweli. Huduma ya elimu na afya ni changamoto kubwa na endelevu katika mchakato wa Uinjilishaji, kwani upungufu wa huduma ya elimu na afya unafungulia milango watu wengi kubaki wakiwa wamezama katika tope la imani potofu, ushirikina na kuabudu miungu wa uwongo kutokana na changamoto za maisha.

Changamoto hii anasema Askofu Kassala kwa uchungu mkubwa, ndiyo lengo la kukidhi hitaji la kutaka kumkomboa mwanadamu mzima: kiroho na kimwili! Jimbo la Geita linataka kusogeza huduma ya afya mjini Geita, itakayokuwa ni msaada mkubwa kwa familia ya Mungu Jimboni Geita! Shule ya Sekondari itakuwa ni kwa ajili ya wasichana na wavulana, kipaumbele cha kwanza kikiwa ni wanafunzi kutoka Geita. Itakuwa pia ni msaada mkubwa kwa watoto wanaohudumiwa kwenye Kituo cha Moyo wa Huruma, Geita, ili kuwapatia wigo mpana zaidi wa kuvuka hali yao ya sasa ili kujipatia elimu itakayowapatia matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Ni matumaini ya Askofu Flavian Matindi Kassala kwamba, huduma makini na endelevu ya elimu na afya itasaidia kuimarisha mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ili kuweza kumjua, kumpenda na kumtumikia Mungu; ni fursa ya kuimarisha imani kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati na kujibu kilio cha maskini kwa mwanga na tunu msingi za Kiinjili. Familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki Geita inaalikwa kuonesha ukarimu kwa Injili, ili kuweza kukamilisha ujenzi wa Hospitali na Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Yohane Paulo II kwa wakati muafaka. Askofu Kassala anawatakia wote paji la elimu katika kudumisha afya na nguvu katika Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.