2017-03-04 15:33:00

Mama Marie Collins ajiengua kutoka kwenye Tume ya Kipapa!


Taarifa iliyotolewa na Tume ya Kipapa ya Kuwalinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia inasema Mama Marie Collins aliyekuwa mwanachama wa Tume hii iliyoanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwezi Machi 2014 ameamua kujiuzuru uanachama wake kuanzia tarehe 1 Machi 2017 kutokana na madai kwamba, kuna baadhi ya viongozi kutoka Vatican ambao wanakwamisha juhudi za Baba Mtakatifu Francisko kupambana dhidi ya nyanyaso za kijinsia.

Kardinali Sean O’Malley, Rais wa Tume hii ya Kipapa amepokea ombi hili kwa masikitiko makubwa na kumwomba Mama Marie Collins kuendelea kutoa ushirikiano wake kwa Tume hata akiwa nje ya tume yenyewe, ombi ambalo amelikubali. Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi hili na kumshukuru Mama Marie Collins kwa mchango na ushirikiano wake tangu alipoteuliwa kuwa mwanachama wa Tume hii ya Kipapa.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu alianzisha Tume hii ili kumpatia ushauri makini utakaosaidia kupambana na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, ili hii kashfa isijirudie tena na hivyo kulichafua Kanisa. Tume hii imepewa dhamana ya kushirikiana na Makanisa Mahalia pamoja na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa ili kuwalinda watoto wadogo dhidi ya uwezekano wa nyanyaso za kijinsia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.