2017-02-28 14:36:00

Mchagueni Mungu chemchemi ya furaha; mali ni kilio na machungu!


Waamini wanahamasishwa kuhakikisha kwamba katika maisha yao wanajitahidi kujiaminisha na kumfuasa Kristo kwa dhati, kwani anawajalia na kuwakirimia mambo msingi wanayohitaji katika maisha, lakini wakimezwa na malimwengu kwa uchu wa mali, fedha, madaraka na anasa, watajichumia mateso, huzuni na mahangaiko ya ndani, kiasi hata cha kukosa amani na utulivu! Waamini wawe na ujasiri wa kujitosa bila ya kujibakiza kama alivyofanya Kristo Yesu, kiasi hata cha kutundikizwa Msalabani.

Kimsingi, waamini hawawezi kumtumikia Mungu na mali ndiyo tafakari ya kina inayotolewa na Mama Kanisa wakati huu, waamini wanapojiandaa kuanza Kipindi cha Kwaresima. Waamini watafakari na kupima uhusiano wao na Mungu pamoja na mali. Kijana tajiri aliyetamani kujisadaka kwa ajili ya kumfuasa Kristo Yesu alishindwa na ”kubwaga manyanga” kwa huzuni kwa sababu alikuwa na mali nyingi! Yesu anawakata maini Mitume wake kwa kuwaambia kwamba, ni rahisi ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.

Mtume Petro akiwa amepigwa bumbuwazi akamswalisha Yesu akisema,”tazama sisi tumeacha yote tukakufuata wewe?” Yesu akamjibu na kumwambia kwenu ninyi mlioacha yote kwa ajili yangu na Injili mtapata maradufu na udhia juu! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 28 Februari 2017 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema Yesu alitaka Mitume wake kuwa na mtindo tofauti kabisa wa kufikiri na kutenda, ili kutambua kwamba, Yesu mwenyewe ndiye sadaka ya kweli na utimilifu wa majitoleo haya unaonekana juu ya Msalaba.

Hii ndiyo njia na dira ya maisha ya Mkristo anayopaswa kuitwaa katika maisha yake hapa duniani, kama ambavyo Nabii Yoshua Bin Sira amefafanua kwenye Somo la kwanza (Rej. YbS 35:1-15) kwa kukazia: ukarimu, sadaka, uchaji wa Mungu, haki, huruma; daima wakimheshimu Mwenyezi Mungu kwa jicho la ukarimu na ukunjufu wa moyo na utimilifu wake ni furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo aliyejisadaka bila ya kujibakiza pale juu Msalabani. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, kijana tajiri hakuwa na ujasiri wa kupokea utimilifu wa maisha kwa kujisadaka kama walivyofanya baadaye Mtakatifu Petro na wenzake. Hata katika shida na magumu ya maisha, Mitume wa Yesu walionesha uso wenye furaha, wasikivu na wenye amani moyoni: Alama makini ya ufuasi wa Kristo!

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa kumkumbuka Mtakatifu Alberto Hurtado aliyefanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi; akajisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini, kiasi hata cha kuwa kweli ni chombo na shuhuda wa Injili ya huduma kwa wananchi wa Chile! Aliteswa na kunyanyaswa, kiasi kwamba, kabla ya kuitupa mkono dunia alisikika akisema, nina furaha na amani katika Bwana. Mtakatifu Hurtardo awe ni mfano bora wa kuigwa kwa waamini wanaotaka kujisadaka bila ya kujibakiza; katika shida na magumu kama kielelezo cha utimilifu wa maisha yao katika Kristo Yesu, wasilalame, bali wawe na ujasiri wa kuridhika na moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.