2017-02-27 13:33:00

Papa Francisko na Askofu mkuu Justin Welby kutembelea Sudan ya Kusini


Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Watakatifu wote, Kanisa Anglikani mjini Roma, Jumapili tarehe 26 Februari 2017 alipata nafasi ya kujibu maswali kadhaa yaliyoulizwa na waamini wa Kanisa Anglikani. Anasema, tangu Mfalme Henri wa VIII alipojitenga na kuanzisha Kanisa Anglikani kumekuwepo na mahangaiko mengi kati ya waamini wa Makanisa haya mawili, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, matukio yote haya yanatafsiriwa kadiri ya historia ya wakati ule. Lakini katika kipindi cha miaka 50 iliyopita kumekuwepo na mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa Anglikani baada ya Askofu mkuu Michael Ramsey kutia sahihi kwenye tamko la pamoja.

Mapokeo ya Makanisa haya mawili, ushuhuda wa watakatifu waliojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, umoja na udugu vimeendelea kujengeka miongoni mwa Wakristo wa Makanisa haya mawili. Kumekuwepo na mshikamano wa dhati kati ya waamini, baada ya mpasuko wa Kanisa unaosababishwa na uchu wa madaraka, nguvu ya kiuchumi na kidini na kwamba, dini ya mtawala, ndiyo dini iliyopaswa kuwa dini ya wananchi wake!  Hii ni sheria ya “Cuius regio eius religio”. Hata katika mpasuko wa kidini, lakini bado waamini waliendelea kushirikiana na kushikamana kwa dhati kwa kutambua kwamba, wao ni wafuasi wa Kristo Yesu. Watawa na Monasteri za kitawa ni nguvu muhimu sana katika maisha ya kiroho na kielelezo makini cha Mapokeo ya Kanisa. Kuna tofauti kubwa kati ya watawa wa Makanisa haya mawili, lakini kwa pamoja wanafanya hija kama wafuasi wa Kristo!

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, katika majadiliano ya kiekumene alikazia zaidi majadiliano ya kitaalimungu kuliko majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma makini! Papa Francisko anakaza kusema, majadiliano ya kiekumene yanafumbatwa katika mchakato wa kutembea na kufanya kazi kwa pamoja, mkazo ambao pia ulitolewa na Mwenyeheri Paulo VI. Majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika taalimungu ni muhimu ili kutambua na kubainisha mizizi ya kinzani iliyopelekea mpasuko na utengano kati ya Wakristo, kwa mfano kuhusu Sakramenti!

Kuna mambo kadhaa ambayo wanataalimungu wanapaswa kuyapatia ufafanuzi ili kuweza kufikia umoja kamili kati ya Wakristo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, anapenda kukazia pia majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Majadiliano ya kiekumene yanafumbatwa katika mchakato wa kujadiliana, kutembea na kufanya kazi kwa pamoja.

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, kuna uhusiano wa karibu sana kati ya Makanisa katika nchi za Kimissionari kama vile Barani Afrika, Asia na Pacific, ikilinganishwa na Makanisa Barani Ulaya. Katika nchi za kimissionari, Ibada ni moto moto, waamini wanajizatiti zaidi katika kipaji cha ugunduzi na ushirikiano wa dhati kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anasema, kwa sasa yeye pamoja na wasaidizi wake wa karibu wanaendelea kuangalia uwezekano wake kutembelea Sudan ya Kusini, huku akiwa ameambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala.

Itakumbukwa kwamba, viongozi wakuu wa Makanisa kutoka Sudan ya Kusini walimtembelea na kuwaomba viongozi wa Makanisa ili waende kushuhudia mateso na mahangaiko ya wananchi wa Sudan ya Kusini, wanaoendelea kupukutika kutokana na vita, njaa na magonjwa. Mashahidi wa Uganda ni mashuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika damu, kama alivyoshuhudia Mwenyeheri Paulo VI alipokuwa nchini Uganda. Ni mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa, waliosimama kidete kiasi hata cha kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo. Kati yao walikuwepo Makatekista kutoka Kanisa Anglikani.

Sehemu mbali mbali za dunia Kanisa Anglikani na Kanisa Katoliki wanashirikiana katika huduma kiasi cha kujenga urafiki na mshikamano kati yao. Wakati mwingine, wanashirikiana hata katika Ibada, kielelezo makini cha utajiri wa maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anasema, itapendeza ikiwa kama Makanisa Barani Ulaya yatawatuma majandokasisi kwenda katika nchi za kimissionari kujifunza uhai na kipaji cha ugunduzi, ili kusaidia mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika ushuhuda wa imani na utambulisho wa Kikristo, ili kumtukuza, kumsifu na kumshukuru Mungu katika maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.