2017-02-27 12:14:00

Papa Francisko atembelea na kusali kwenye Kanisa Anglikani Roma!


Kwa mara ya kwanza katika historia, Kanisa Anglikani lilianza kutoa huduma ya Liturujia mjini Roma miaka 200 iliyopita. Tangu wakati huo, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika mahusiano kati ya Kanisa Anglikani na Kanisa Katoliki. Hali ya kudhaniana na vibaya, chuki na uhasama kati ya waamini wa Makanisa haya mawili imepitwa na wakati, kwa neema ya Mungu, waamini hawa sasa wanaangaliana kama ndugu katika Kristo, udugu unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo.

Waamini hawa wanatambuana kama marafiki na mahujaji wanaopaswa kusafiri  pamoja, ili kumfuasa Kristo Yesu. Sanamu ya Yesu Mkombozi wa Ulimwengu inawangalia kwa jicho la ukombozi, huruma na upendo. Ni jicho lile lile la upendo lililowangalia na kuwagusa Mitume wa Yesu, kiasi hata cha kuamua kuacha yote na kumfuasa Kristo, changamoto na mwaliko kwa wafuasi wa Kristo hata leo hii kujibu changamoto hii kutoka kwa Kristo, ikiwa kama kweli wanataka kuacha yote ya nyuma na kuanza kumwambata; ili huruma na upendo wake viweze kufahamika na wengi!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 26 Februari 2017 wakati wa Ibada ya pamoja na waamini wa Kanisa Anglikani, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 tangu Parokia ya Wakatifu wote, Kanisa Anglikani ilipoanzishwa. Kwa mara ya kwanza katika historia, Khalifa wa Mtakatifu Petro ametembelea Kanisa Anglikani mjini Roma. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huruma ya Mungu ni kiini cha utume wa Kikristo na kwa sababu hiyo, kwa kuwa wana huduma hii, kwa jinsi walivyopata rehema kwa Mwenyezi Mungu kamwe hawawezi kulegea. Huduma yao inabubujika kutoka katika huruma ya Mungu inayowainua na kuwategemeza ili wasipoteze ari na mwamko huo.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Paulo hakuwa na mahusiano mazuri sana na Wakristo wa Korintho, wakati mwingine alitembelea Jumuiya hii ya waamini kwa uchungu na masikitiko makubwa yanayoshuhudiwa katika Nyaraka zake. Katika kuishi utume wake kwa mwanga wa huruma ya Mungu, Paulo anaonesha jinsi ambavyo alifanikiwa kuvuka tofauti zilizojitokeza huko siku za nyuma, hakatishwi tamaa na kinzani pamoja na migawanyiko inayojitokeza kati ya Wakristo. Mtume Paulo akajizatiti katika mchakato wa upatanisho, changamoto kwa Wakristo kukimbilia Uso wa Yesu mwenyewe huruma, ili awasaidie kukivuka kipindi hiki kigumu, na hivi ndivyo Wakatoliki na Waanglikani wanavyofanya kwa wakati huu kama walivyofanya Wakristo kwenye Jumuiya zile za kwanza!

Mtume Paulo aliweza kutekeleza dhamana hii kwa njia ya unyenyekevu, ambao kimsingi ni fadhila njema na utambulisho wa mtu. Paulo anajiona kuwa kama Mtumishi aliyetumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu na Bwana mleta uzima. Anatekeleza dhamana hii kutokana na huruma aliyoonjeshwa na Mwenyezi Mungu na wala si kwa nguvu na jeuri yake binafsi, bali kwa kujiaminisha mbele ya Mungu anayemwinua kutoka katika unyonge wake kwa njia ya huruma. Mtu anapojinyenyekesha anaonesha kwamba, anakimbilia huruma ya Mungu katika maisha na utume wake, na mwanzo wa Mungu kuanza kutenda kazi ndani ya watu wake. Mchakato wa Uinjilishaji mpya unawataka Wakristo kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu kama kipaumbele chao cha kwanza ili waweze kuwashirikisha walimwengu furaha ya kupenda na kupendwa na Kristo Yesu.

Wakristo wanakumbushwa kwamba,  wamepewa hazina hii katika vyombo vya udongo ili adhama kuu ya uwezo iwe ni ya Mungu. Paulo, mdhambi aliyetubu na kuongoka anatambua kwamba alikuwa dhaifu sana, lakini huruma ya Mungu imetenda maajabu makubwa katika maisha yake na sasa anahesabika kuwa ni kati ya Mitume mashuhuri wa Yesu. Wakristo wakitambua udhaifu wao na kuomba msamaha, huruma ya Mungu inayoponya itawashukia na kung’ara katika maisha yao, kiasi hata cha Uso wa huruma ya Mungu kuonekana hata na wale waliko nje. Kinzani na mipasuko anasema Baba Mtakatifu ni sehemu ya maisha ya binadamu, lakini haina uamuzi wa mwisho.

Uhusiano kati ya Mtume Paulo na Wakristo wa Korintho uliweza kurekebishwa kiasi kwamba, akafanikiwa kupeleka msaada uliokuwa umetolewa na Kanisa la Yerusalemu. Wakristo wa Korintho wakapata mwamko mpya na kuanza kushirikiana kutoa huduma kwa wahitaji. Hii ndiyo dira na mwelekeo unaooneshwa na Kanisa Anglikani mjini katika huduma kwa maskini wanaoishi mjini Roma. Umoja na mshikamano wa kweli unaundwa na watu wanaofanya kazi kwa kushirikiana ili kutoa huduma kwa maskini, ushuhuda wa upendo na Uso wa huruma wa Yesu unaojionesha kati ya watu wa mji wa Roma.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, baada ya miaka yote hii ya kutoelewana kati ya Waamini wa Kanisa Anglikani na Wakatoliki, hatimaye, wameanza kutambua na kuonja neema ya Mungu inayotenda kazi ndani mwao; kiasi kwamba, tamaa ya kuwa karibu zaidi katika sala na ushuhuda wa Injili inajionesha katika huduma mbali mbali kwa watu. Safari ya majadiliano ya kiekumene inaweza kuonekana kana kwamba, inakwenda mwendo wa “kinyonga”, lakini wanatiwa moyo kwa kukutana na kusali pamoja. Kwa mara ya kwanza, katika historia, Papa anatembelea Kanisa Anglikani mjini Roma, kielelezo cha neema na uwajibikaji ili kuimarisha uhusiano wao na kumtukuza Kristo Yesu kwa njia ya huduma ya Injili kwa ajili ya mji wa Roma.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa mahubiri yake, anawaalika Wakristo wote kuomba neema ya kuwa mitume waaminifu wa Kristo; kwa kuondokana na maamuzi mbele ambayo kwa miaka mingi yamejikita katika historia. Ushirikiano kati ya Parokia ya Watakatifu Wote, Kanisa Anglikani na Parokia ya Watakatifu wote Kanisa Katoliki ni mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watakatifu wa Kanisa wanaoungana kwenye Yerusalemu ya mbinguni wasaidie mchakato wa kujenga na kudumisha udugu na safari ya maisha ya Kikristo, kwani wote wamekusanyika kwa jina la Yesu anayewangalia kwa jicho la huruma; akiwataka kujizatiti zaidi katika ujenzi wa umoja na upendo miongoni mwa Wakristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.