2017-02-27 15:00:00

Majadiliano ya kiekumene katika huduma kwa maskini!


Mchungaji Jonathan Boardman wa Kanisa Anglikani, Jumapili tarehe 26 Februari 2017, kwa niaba ya waamini wa Parokia ya Kanisa la Watakatifu Wote, Mjini Roma, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kupamba Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Watakatifu wote mjini Roma. Anasema, mwanzoni, walipokuwa wanatumia cheo cha “Askofu wa Roma” kilijengeka katika dharau, lakini leo hii, cheo hiki kina mwelekeo na tafsiri mpya ya Papa Francisko anayeshuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake kwa kuwa kati pamoja na watu wake. Amekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa kama shuhuda wa Injili na kiongozi wa Kanisa la Kristo.

Bado anakumbuka mahubiri ya huruma ya Mungu, wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya Kristo Mchungaji mwema, alivyofafanua Injili kuhusu huruma ya Mungu kwa waja wake. Mtakatifu Yohane XXIII alipotembelewa na Askofu mkuu Fisher alimwonesha kwa taabu kubwa giza lililokuwa linawafumbata waamini wa mji wa Roma, lakini hija yake ya kichungaji Parokiani hapo ni kielelezo cha ushuhuda wa mwanga wa Kristo unaonesha dira na njia ya kufuata ili kutekeleza mapenzi ya Mungu, huku Wakristo wote wakiwa wameungana pamoja! Wakristo na Waangalikani wanajivunia kuunganishwa na Mtakatifu Beda. Lakini Mtakatifu George Herbert ambaye pengine hafahamiki sana na mahujaji kutoka katika Makanisa mengine, lakini ni maarufu sana kwa Kanisa Anglikani. Alikuwa ni mtunzi mashuhuri wa mashairi yanayofafanua imani ya Kikristo inayomwilishwa katika huduma za kichungaji. Mashairi yake ni mwaliko wa kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha, kwani Hekalu ni dirisha la neema ya Mungu kwa waja wake na watakatifu ni mashuhuda na watangazaji wa mwanga na utukufu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.