2017-02-27 14:41:00

Kanisa Anglikani linampongeza Papa Francisko kwa huduma kwa maskini


Askofu Robert Innes wa Kanisa Anglikani, Jimbo la Ulaya, Jumapili tarehe 26 Februari 2017 alimkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Kanisa la Watakatifu wote mjini Roma, akiweka historia ya kuwa ni Papa wa kwanza kutembelea Kanisa Anglikani. Lakini, ikumbukwe kwamba, kuna uhusiano mwema kati ya viongozi wakuu wa Makanisa haya kama ilivyojionesha kwa Askofu mkuu Justin Welby kukutana na kuzungumza na Papa Francisko mara tatu tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kunako mwaka 2013.

Hivi karibuni, viongozi hawa wawili waliweza kusali pamoja Masifu ya Jioni kwenye Kanisa “San Gregorio al Cielo” na hapo Papa Francisko alimpatia zawadi ya Fimbo ya Kiaskofu iliyotolewa na Papa Gregory mkuu kwa Mtakatifu Augustino, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cantebury. Viongozi wengi wa Kanisa Anglikani, bado wanalikumbuka tukio hili la kihistoria! Askofu Innes ametumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uongozi makini unaoshuhudiwa na Papa Francisko, hasa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Papa Francisko amekuwa ni kiongozi anayejipambanua katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo.

Papa Francisko ameendelea kutoa changamoto kwa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kuvumbua tena urithi, tunu msingi za maisha na amana yao kutoka katika Ukristo. Mafundisho ya Baba Mtakatifu katika medani mbali mbali za maisha yamekuwa na mafao makubwa kwani ni mafundisho yanayogusia kwa kiasi kikubwa changamoto za kimaadili na utu wema, zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Askofu Robert Innes wa Kanisa Anglikani, Jimbo la Ulaya, anahitimisha hotuba ya kumkaribisha Baba Mtakatifu kwenye Kanisa la Watakatifu wote mjini Roma, kwa kutumaini kwamba, hatua hii itasaidia kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kuimarisha umoja na mshikamano kati ya Waamini wa Kanisa Anglikani na Wakatoliki kwa ajili ya mafao ya wengi!

Wakati huo huo, katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Kanisa la Watakatifu Wote mjini Roma, Parokia hii kwa kushirikiana na Parokia ya Watakatifu wote Jimbo Kuu la Roma, wameamua kushirikiana kiuchumi ili kuwasaidia maskini kwa chakula cha jioni, wale wanaopata hifadhi kwenye Kituo cha Treni cha Ostiense mjini Roma kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko. Katika maadhimisho haya, Kanisa Anglikani limeamua kuchapisha Biblia 200 na kati yake Biblia 50 zitatolewa zawadi kwa mtandao wa watawa unaopambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.