2017-02-27 15:25:00

Jifunzeni kufanya maamuzi machungu katika maisha! Kusuka au kunyoa!


Leo changamoto kuwa ni“Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini, wala miili yenu, mvae nini.” ni maneno ya Yesu yanayotuacha midomo wazi siku ya leo, kwani yanazungumza juu ya mahangaiko yanayoisonga mioyo ya wengi. Utawezaje kuwahubiria watu fukara au hata matajiri maneno haya eti: “msisumbukie maisha yenu.” Yatubidi tuyatafakari zaidi maneno haya na kuyaelewa kiundani ili kujua Yesu eleweke kwamba Yesu hatuambii kutohangaika kutafuta chakula na mavazi aihda hatualiki kujibweteka bila kazi na kumwomba Mungu afanye muujiza wa kututatulia matatizo yetu. La hasha, bali yabidi tujikwinde kujitatulia matatizo yetu sisi wenyewe.

Yesu anazungumzia mahitaji ya msingi mawili yanayotusukuma na kuyahangaikia katika maisha, yaani chakula na mavazi. Ama kweli mtu hawezi ukaishi bila chakula na bila kuvaa. Kwa vyovyote Yesu anapotamka chakula hamaanishi ugali, wali, matoke “chips dume”, “Malalanje” au mkate peke yake, bali anamaanisha kila aina ya lishe tunayohitaji katika maisha. Watu tunahitaji aina nyingine zaidi ya chakula ili kuwa binadamu halisi katika maisha yetu. Mathalani, tunahitaji kuwa na ujuzi wa mambo, tunahitaji afya njema, tunahitaji kujua mambo, tunahitaji kupendwa nk.

Hizi ndizo njaa tunazozihangaikia na kuzisumbukia. Kadhalika kuhusu mavazi, Yesu hamaanishi nguo tu ya kujifunika na kujisitiri mwili, bali kila aina ya nguo inayotusetiri tunapotokea mbele ya kadamnasi. Bali hata viwalo tunavyovitundika maungoni tunapotaka kujitokeza kujionesha kadamnasi kuwa tu watu wa hadhi gani katika jamii. Kwa hiyo kama tunatafuta chakula na mavazi kwa mahangaiko, hapo maana yake tunakosa mlingano wa ndani katika maisha yetu hivi kuna kitu fulani hakiendi sawasawa katika fikra zetu. Kwa hiyo tunaalikwa kujipatanisha na sisi wenyewe, kujipatanisha na Mungu na ndugu zetu.

Kabla ya kuziona hoja za kutuonya tusihangaikie chakula na mavazi, Yesu anazungumzima juu ya maamuzi ya maisha yetu anasema: “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu:” Neno la kiaramayo lenye maana ya mali ni mamona. Mzizi wake ni emuna maana yake ni imani. Mamona ni kitu anachojiaminisha kabisa binadamu na kutolea maisha yote. Hapa Yesu amechukua mazingira ya kijamii ya kawaida ya mtumishi wa nyumba. Mtumishi hawezi kutumikia mabwana wawili. Kulikuwa pia msemo mwingine wa Wayahudi uliosema: “Huwezi kukwea farasi wawili wakati mmoja.” Kumbe, waswahili tunasema: “njia mbili zilimpasua mzee fisi msamba.” Yesu anasema: “hamwezi kumtukia Mungu na mali,” yaani inabidi kuchagua jambo moja katika maisha na kujizatiti nalo.

Nabii Eliya aliwaambia Waisraeli: “Mtasitasita katikati ya mawazo mawili hata lini?” (IWaf. 18:21). Kwa hiyo mkristo yambidi  amchague Kristo na kuaminisha maisha yake yote kwake. Kisha Yesu anatoa hoja zake kwa nini tusihangaikie, tusisumbukie. Hoja ya kwanza Yesu anasema: “je, maisha si zaidi ya chakula na mwili zaidi ya mavazi?” Yaani yabidi kuangalia, kwamba kuna kitu muhimu zaidi ya maisha haya ya kibaolojia. Maisha hayo ni tata, kwani unaweza kujidhani unaishi maisha mazuri, unakula vizuri, unalala vizuri, unavaa vizuri, lakini mwishoni unabaki kujiuliza, kwa sababu gani nimeishi. Kwa fikara anayotupatia Yesu, ni kujiuliza kwa nini ninaishi hapa duniani, na kwamba vitu hivi siyo hatima ya mwisho ya maisha.

Hoja ya pili Yesu anasema: “Waangalieni ndege wa angani,” hatuambii “tufanye kama ndege wa angani” la hasha bali anasema: “waangalieni ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni”  Aidha hasemi “Baba yao wa mbinguni,” bali anasema “Baba yenu huwalisha hao. Ninyi je, si bora kupita hao?” Hii ndiyo hoja inayotufanya tuondoe mahangaiko. vinginevyo wewe huamini kwamba kuna Mungu anayekupenda na anayeyapa maisha yako umaana. Kadhalika anasema: “Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo, hayafanyi kazi, wala hayasokoti.” Hapa Yesu anatumia maelezo ambayo yaonekana yalikuwa yanaeleweka kabisa kwa watu wake, hasa pale alipohamisha makazi yake kutoka Nazareti hadi Kafarnaumu. Kwani kandokando ya ziwa la Galilea kuna aina ya mimea iliyostawi vizuri na inayotoa maua yanayopendeza.

Yesu anataka kutufikirisha na kututafakarisha mpango wa upendo wa Mungu, kwamba ameumba vizuri kila kitu na kutupatia maana ya maisha yetu. Tofauti kati ya mtu anayeamini na asiyeamini, si kwamba mmoja nafanya kazi na mwingine hafanyi kazi, la hasha, bali wote kufanya kazi bali tofauti ni hii kwamba anayeamini anajua kuna Baba anayempa maana ya maisha yake, na hali inayo inampa amani na kumwondolea mahangaiko. Ndugu zangu, leo tunaaswa na Yesu kwamba yatubidi tuwajibike katika ulimwengu huu, lakini tusihangaikie wala kutaabikia mamona ya ulimwengu huu. Tuhangaike kupata mahitaji yetu ya chakula na mavazi, kwa ajili ya Mungu na watu wake.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.