2017-02-21 07:45:00

Jubilei ya Miaka 100 tangu B. Maria alipowatokea Watoto wa Fatima


Baba Mtakatifu Francisko katika kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, yaani: Francis, Yacinta na Lucia, kuanzia tarehe 12- 13 Mei 2017 atakuwa na hija ya kitume nchini Ureno, kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima. Nembo na kauli mbiu ya maadhimisho haya tayari imetolewa na kamati kuu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima. “Papa Francisko mjini Fatima 2017 pamoja na Bikira Maria kama mahujaji wa matumaini na amani”.

Kwa namna ya pekee kabisa, waamini wanaalikwa kudumisha Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili; ili kujiachilia wazi mbele ya Mwenyezi Mungu, tayari kujazwa na upendo wake usiokuwa na kifani. Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu. Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima aliwaagiza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani na amani duniani.

Padre Carlos Cabecinhas, Mratibu mkuu wa Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Ureno anakaza kusema, haya ni mambo makuu ambayo familia ya Mungu nchini Ureno inapenda kuyapatia uzito wa pekee wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima. Kumbe, toba, wongofu wa ndani, amani na huruma ni mambo ambayo pia yanapewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Padre Carlos Cabecinhas anahitimisha kwa kusema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Ureno itamwezesha kusali na familia ya Mungu nchini Ureno pamoja na bahari ya mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi kubwa ya Fatima kwa Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.