2017-02-18 15:46:00

Sinema ya wagonjwa wa Hospitali ya Watoto ya Bambino Gesù


Ugonjwa na mateso yamekuwa daima kati ya matatizo mazito sana yanayoyaweka maisha ya mwanadamu katika majaribu. Katika ugonjwa mtu anapata mang’amuzi ya udhaifu na ukomo wake kama binadamu! Ugonjwa unamfanya mwanadamu kuchungulia kaburi! Ugonjwa unaweza kuwa ni sehemu ya mahangiko makubwa ya binadamu, kiasi hata cha kukata tamaa na kumwasi Mwenyezi Mungu. Lakini, ugonjwa ukichukuliwa kwa imani na matumaini, ni shule ya maisha inayoweza kumkomaza mtu, ikamsaidia kupambanua mambo msingi katika maisha. Mara nyingi wanasema Mababa wa Kanisa ugonjwa huchochea ile hamu na ari ya kumtafuta Mungu, ili kuweza kurejea tena kwake!

Kituo cha Televisheni cha Taifa nchini Italia RAI 3 kuanzia tarehe 19 Februari 2017 kitaanza kurusha Sinema ya maisha ya watoto wagonjwa wanaotibiwa kwenye Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Hii ni sinema ya maisha ya watoto wanaosumbuliwa na magonjwa makubwa; familia zao pamoja na wafanyakazi wa afya wanaowahudumia kama mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Ni sinema inayogusa Fumbo la maisha na kifo cha binadamu. Watoto hawa kumi pamoja na wale wote wanaowahudumia wanapambana na fumbo la kifo katika hali ya udhaifu wao; ujasiri, machozi na tabasamu la kukata na shoka, kiasi hata cha kuthubutu kusimulia hali yao ya ndani kama changamoto ya mapambano dhidi ya kifo! Hii ni sehemu ya habari njema kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake kwa Siku ya 51 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni.

Baba Mtakatifu anawataka wadau katika tasnia ya habari kuandika na kutangaza matukio yanayoendelea kujiri dunia kwa mwanga wa matumaini yanayofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu, ili kugusa madonda, mateso na mahangaiko ya mwanadamu katika mwanga wa Injili. Hii ni changamoto ya kuondokana na tabia ya kupenda kushabikia sana “habari za udaku”. Lengo ni kuvuka woga na wasi wasi usiokuwa na mashiko kwa kujikita katika habari njema inayoamsha matumaini; kwa kuwataka wadau mbali mbali kujizatiti ili kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Hii ni sehemu ya utangulizi wa Sinema ya Watoto wa Hospitali ya Bambino Gesù, unaosimuliwa na Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sektretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican anayekaza kwa kusema, mwanadamu anayeweza kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto za maisha na hatimaye kupata ushindi ikiwa kama wameungana! Sinema hii inaonesha kwamba, inawezekana mtu akawa mgonjwa, lakini bado akaendelea kuwa na amani na utulivu wa ndani, kielelezo makini cha matumaini na huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Hii si mara ya kwanza kwamba, Sinema inaonesha mateso na mahangaiko ya mwanadamu katika magonjwa kwani tayari kuna sinema kadhaa zimewahi kuchezwa kuhusiana na ugonjwa wa Ukimwi, Saratani pamoja na magonjwa mengine makubwa makubwa duniani. Sinema hizi zinazungumzia ugonjwa, ili kuwatafakarisha watu kuhusu elimuviumbe maadili; kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema unaofumbatwa katika sinema. 

Magonjwa pia yamekuwa ni sababu ya watu kuachishwa kazi ili kuwatunza wapendwa wao! Hii ni changamoto inayoonesha ugonjwa daima ni sehemu ya Fumbo la maisha ya binadamu, linaloweza kupata maana ya pekee kwa kukutana na Kristo Yesu katika mahangaiko ya binadamu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya wagonjwa duniani kwa mwaka 2017, iliyoadhimishwa hivi karibuni huko Lourdes, Ufaransa. Kitanda cha mgonjwa, hospitali au mahali ambapo mgonjwa anapewa tiba inaweza kuwa ni fursa ya kujenga madaraja ya kukutana na watu, ili kudumisha amani na mshikamano wa upendo kati ya wagonjwa, familia zao pamoja wafanyakazi katika sekta ya afya anasema Baba Mtakatifu, ili kuvuka vikwazo na migawanyiko.

Katika miaka ya hivi karibuni anasema  Monsinyo Dario Edoardo Viganò kwamba, watoto, vijana na magonjwa imekuwa ni kati ya tema ambazo zimefanyiwa kazi kwa kina na mapana katika ulimwengu wa televishen. Licha ya magonjwa kuendelea kuwaandama watoto na vijana hawa, lakini wao wanataka kusonga mbele na kuendelea kuota ndoto ya maisha bora zaidi kwani wanatambua kwamba, ugonjwa hauna neno la mwisho, badala yake Injili ya uhai inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza; kwa kupenda na kuwa na imani kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Sinema ya watoto wa Hospitali ya Bambino Gesù ni mashuhuda na vyombo madhubuti vinavyomwimbia Mungu utenzi wa maisha licha ya mateso na maumivu yao kutokana na magonjwa yanayowasibu. Huu ni mwanga wa Injili unaofukuzia mbali giza la maisha na hali ya kukata tamaa. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwamba: maisha ya binadamu ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kusimuliwa kwa kuzingatia mambo msingi, ili kuweza kuona ukweli wa mambo. Changamoto ya ugonjwa katika maisha ya binadamu anasema Monsinyo Eduardo Viganò ni endelevu, inayofumbatwa katika tabasamu la kukata na shoka na matumaini ya kuweza kupona na kurejea katika hali ya maisha ya kawaida.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.