2017-02-17 14:15:00

Papa Francisko: Dhamana na wajibu wa Chuo kikuu!


Elimu na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya ni changamoto inayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya maisha na maendeleo endelevu ya jamii husika. Mshikamano wa huduma na upendo ni chachu makini ya ujenzi wa utamaduni wa Kikristo. Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ni mahali muafaka pa mshikamano wa ujenzi wa jamii dhidi ya umaskini wa kijamii kwa kushirikiana na kuamianiana katika maisha. Vijana wanatakiwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Kristo kwa watu wanaowazunguka. Mshikamano wa dhati unapingana na wasi wasi usiokuwa na mvuto wala mashiko na matokeo yake unasaidia kukuza na kudumisha majadiliano, utu na heshima ya binadamu.

Kimsingi huu ni muhtasari wa hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 17 Februari 2017 alipotembelea Chuo Kikuu cha Roma Tre” na kujibu maswali manne kutoka kwa wanafunzi chuoni hapo. Baba Mtakatifu anasema, Jamii imebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa mambo mazuri, matendo ya mshikamano na upendo kwa jirani. Kuna makundi makubwa ya watu wanaojisasaka kwa ajili ya kutoa huduma kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; alama inayotia moyo, hata kama jamii bado inazungukwa na vitendo ya uadui, kinzani na matumizi ya nguvu.

Inaonekana kana kwamba, watu wako katika Vita Kuu ya Tatu ya Dunia, kwani kuna vita na kinzani sehemu mbali mbali za dunia, kiasi hata cha kutishia usalama wa maisha kwa siku za usoni. Lakini, jambo la kushangaza ni kuona kwamba, sera na mikakati inayotolewa na Jumuiya ya Kimataifa haijafanikiwa bado kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Kumbe, Chuo kikuu ni mahali ambapo dhamiri nyofu inaundwa, ili kutafuta na kusimamia kile kilicho chema! Lakini kwa bahati mbaya, biashara haramu ya silaha duniani inaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia. Kuna mamilioni ya watu wanaokufa kwa baa la njaa, magonjwa na umaskini, kashfa kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Licha ya changamoto zote hizi anasema Baba Mtakatifu, hakuna sababu msingi ya kukata tamaa hasa miongoni mwa vijana, kwani kufanya hivyo ni kukosa hata mwelekeo wa maisha.  Vijana wanatakiwa kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha badala ya kukimbilia katika furaha za mpito ambazo mara nyingi zinawasababishia majonzi makubwa katika maisha. Mabomu yanaendelea kusababisha vifo; matumizi haramu ya dawa za kulevya yanaharibu afya ya akili, mwili na roho na matokeo yake ni ulevi wa michezo ya kamali inayosambaratisha maisha ya vijana wengi. Chuo kikuu ni mahali pa kupambana dhidi matumizi haramu ya dawa za kulevya yanayosababisha madhara makubwa kwa watu, familia pamoja na gharama kubwa kwa jamii.

Baba Mtakatifu anawataka wanafunzi wa Chuo kikuu kuhakikisha kwamba, wanachakarika usiku na mchana kushirikiana na wengine kwa ajili ya kutoa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kudumisha uzalendo. Kuna changamoto kubwa ya umaskini, kiasi kwamba kuna umati mkubwa wa watu wasiokuwa na makazi, wanaolazimika kulala pembeni mwa barabara; kuna wakimbizi na wahamiaji; kimsingi kuna umaskini mkubwa wa kijamii unaopaswa kuamsha dhamiri ya watu wanaopandikiza utamaduni wa kifo, anasa na starehe za kupindukia; watu wenye uchu wa mali, fedha na madaraka! Watu wawe na ujasiri wa kujenga madaraja ya mshikamano, kwa kuaminiana na kuthaminiana katika maisha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mazingira ya Chuo kikuu yanapaswa kuwa ni mahali ambapo wanafunzi wanapata nafasi ya kutafakari na kufanya mang’amuzi ya kina kwa kuwa na upeo mpana zaidi. Mageuzi makubwa yanahitaji mwelekeo mpya wa sera na mifumo ya: kiuchumi, kitamaduni na kijamii, kwa kumweka binadamu kuwa ni kiini cha mageuzi yote haya. Lengo ni kujenga utandawazi wa mshikamano unaofumbatwa katika kanuni maadili na maisha ya kiroho; kwa kutafuta kilicho chema na kizuri kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu Francisko katika ushuhuda wake anasema, ni Mkristo na Mfuasi amini wa Kristo Yesu na kwamba, Injili yake ni nguvu ya kweli inayoweza kupyaisha maisha ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake. Anazungumza si kwa sababu anataka kuwaongoa bali ni kwa vile amekutana na Kristo Yesu akamletea mabadiliko na kumwonesha upeo mpana na hivyo kuwa ni chemchemi ya furaha na maana halisi ya maisha yake. Yesu amekuwa ni mwenza mwaminifu wa safari ya maisha na kamwe hawezi kumsaliti au kumdanganya mtu awaye yote.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa maisha yao ya kiimani bila kuogopa kukutana na Kristo Yesu, ili kujenga na kuimarisha urafiki; kwa njia ya imani thabiti pamoja na kuwa na mwelekeo sahihi wa binadamu. Kwa kuambatana na Kristo Yesu si kwamba, matatizo na changamoto za maisha zinapewa kisogo la hasha! Bali mtu anapata nafasi ya kuangalia mambo bila wasi wasi kwa kukabiliana na changamoto zote za maisha katika Mwanga wa Injili. Chuo kikuu kinaweza kuwa ni mahali pa kufunda wafanyakazi wa upendo wa akili; kwani Chuo kikuu ni mahali pa majiundo ya hekima yanayotoa kipaumbele cha kwanza kwa maendeleo endelevu ya mtu: kiroho na kimwili; chuo kikuu ni chachu ya upyaisho wa jamii!.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Chuo kikuu kinaweza kuwa ni mahali pa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na ukarimu kwa watu wenye tamaduni na imani tofauti. Kinzani na mipasuko dhidi ya utamadui wa Kikristo vinapata chanzo chake Barani Ulaya; kwa kujifungia katika ubinafsi, utamaduni pasi na matumaini ya kupyaisha jamii na tamaduni zake. Utamaduni unakua na kupanuka kwa kujikita katika kanuni na tunu zake msingi.

Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Chuo kikuu cha Roma Tre kujenga na kuishi katika mazingira ya majadiliano ya kweli katika utofauti hata pale kunapotokea kinzani, zisaidie kuwa na mwelekeo bora zaidi; kwa kuthamini na kuenzi tunu za watu wengine ili kuvuka kishawishi cha kutowajali wengine na wasi wasi usiokuwa na mashiko wala mvuto! Chuo kikuu kiwe ni mahali pa watu kukutana, kujadiliana na kukongamana! Mahali pa ujenzi wa ujuzi na maarifa yanayofumbatwa katika mshikamano unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Hiki ndicho kiini cha amani, matumaini kwa kila nchi na ulimwengu katika ujumla wake. Kwa wafanyakazi na wanafunzi wa chuo kikuu wanapaswa kuacha kumbu kumbu nzuri katika historia. Mwishoni Baba Mtakatifu anasema, matumaini yawe ni mwanga unaoyaangazia masomo na dhamana yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.