2017-02-16 15:43:00

Kumbu kumbu ya Miaka 88 ya Mkataba wa Laterano: Mafao ya wengi!


Wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi Barani Ulaya pamoja na changamoto za kijamii zinazoendelea kujitokeza ndani na nje ya Italia ni kati ya tema zilizojadiliwa hivi karibuni kati ya ujumbe wa viongozi wakuu 16 kutoka Vatican ulioongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican pamoja na Serikali ya Italia waliokuwa chini ya uongozi wa Rais Sergio Mattarella, kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 88 tangu Serikali ya Italia na Vatican walipotiliana sahihi kwenye Mkataba wa Laterani na huo ukawa ni mwanzo wa kuundwa kwa Serikali ya Vatican inayojitegemea kwa mambo yake, chimbuko la uhuru wa Kanisa.

Mkataba wa Laterano ulitiwa sahihi kunako tarehe 11 Februari 1929 na kufanyiwa Marekebisho kunako tarehe 18 Februari 1984. Maadhimisho haya anasema Kardinali Parolin yamekwenda vyema kwa kupembua tema ambazo zina mashiko kwa Vatican na Italia katika ujumla wake; kuna mambo msingi ambayo pande hizi mbili zinakubaliana lakini pia kuna mambo ambayo wanatofautiana kimsingi, lakini yote yanatendeka katika hali ya amani na utulivu, kwani lengo ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Italia.

Kwa sasa kilio kikubwa cha vijana wa kizazi kipya ni ukosefu wa fursa za ajira na matokeo yake kuna baadhi ya wanasiasa wanataka kutumia mwanya huu ili kujijenga kisiasa, kama ilivyo pia kwa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora Barani Ulaya. Kuna baadhi ya wanasiasa wanapenda kutumia changamoto hii kutishia usalama na maisha ya wananchi wa Italia jambo ambalo halina msingi wowote.

Hapa kuna haja ya kujenga madaraka ya watu kukutana na kusaidiana anasema Kardinali Parolin, badala ya kujifungia katika ubinafsi, kwani hiki ni kielelezo cha siasa chafu zisizo na mvuto wala mashiko kwa watu. Umuhimu wa kuwasaidia na kuwahudumia watu walioathirika kwa tetemeko la ardhi nchini Italia ni kati ya mambo ambayo pia yalipewa msukumo wa pekee, ili kuanza tena mchakato wa ujenzi wa maeneo haya si tu kwa kuangalia miundo mbinu, bali hata kimaadili na kiutu.

Roma inajiandaa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu Umoja wa Ulaya ulipoanzishwa, changamoto kubwa iliyoko mbele yao ni kujenga umoja na mshikamano wa dhati; kwa njia ya upyaisho wa ndani utakaowasaidia viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya kusoma alama za nyakati kwa kuibua sera na mikakati makini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hapa kuna haja ya kujikita katika tunu msingi zinazofumbatwa katika ujenzi wa Umoja wa Ulaya; kwa kukazia pia haki na wajibu wa raia wa Umoja wa Ulaya. Ujumbe wa Vatican umeonesha wasi wasi wake kuhusu muswada wa sheria inayokumbatia utamaduni wa kifo na kwamba, kuna haja ya kufanya majadiliano ya kina kati ya daktari na mgonjwa kwa kukumbuka kwamba maisha ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumbe inapaswa kulindwa na kudumishwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu! Utamaduni wa kifo ni janga kwa ustawi na maendeleo ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.