2017-02-16 07:31:00

Baraza la Makardinali Washauri lahitimisha mkutano wake wa XVIII


Baraza la Makardinali washauri katika mkutano wake wa XVIII chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 13- 15 Februari 2017 limepembua kwa kina na mapana “huduma ya haki” inayogusa kwa namna ya pekee shughuli na utume unaofanywa na “Toba ya Kitume”, “Mahakama kuu ya Kanisa Katoliki” pamoja na “Mahakama kuu ya Rufaa ya Kitume”. Katika mkutano huu, Makardinali wanasema wanaunga mkono mchakato wa mageuzi unaoendelea kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo!

Makardinali katika mkutano wao kadiri ya taarifa iliyotolewa na Dr. Paloma Garcia Ovejero, Msemaji mkuu msaidizi wa Vatican, kwa vyombo vya habari, Jumatano, tarehe 15 Februari 2017 anasema, Makardinali wameendelea kuchangia kuhusu mabaraza mbali mbali ya Kipapa kwa kuangalia: Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu; Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki pamoja na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini. Makardinali wote washauri wamehudhuria pamoja na kushiriki na Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican wakati wote wa mkutano wao.

Kati ya tema zilizojadiliwa ni pamoja na mchakato wa sifa kwa ajili ya Mapadre wanaofaa kuteuliwa kuwa Maaskofu, ili kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu watakaokabidhiwa kwao na Mama Kanisa. Mada hii imekwisha pembuliwa kwenye mikutano ya nyumba, sasa imechambuliwa na mapendekezo kuwasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya maamuzi zaidi. Kardinali George Pell amewaelezea Makardinali washauri kuhusu kukamilika kwa mchakato mzima wa mageuzi ya uchumi kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Hapa mkazo umewekwa kwenye rasilimali watu na nguvu kazi, ili kuhakikisha kwamba wanapata majiundo makini ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kuzingatia kanuni, sheria, tija na weledi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo!

Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican amewasilisha mbele ya Baraza la Makardinali washauri, hatua mbali mbali ambazo zimekwisha kuchukuliwa na Sekretarieti hii kama sehemu ya utekelezaji wa mageuzi kwenye vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Tayari Radio Vatican na Kituo cha Televisheni cha Vatican vimeunganishwa. Kuna mabadiliko makubwa katika mgawanyo wa masafa ya kurushia matangazo kutoka Radio Vatican pamoja na sera mpya zitakazotumika kwenye mitandao ya kijamii. Tayari mchakato wa mageuzi kwenye Kitengo cha Uchapaji cha Vatican umeanza kufanyiwa kazi. Mwishoni, Baraza la Makardinali washauri litakutana tena kuanzia tarehe 24 – 27 Aprili 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.