2017-02-15 12:41:00

Mahakama mpya kuzinduliwa kwa ajili ya watoto huko Zanzibar


Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limesema Zanzibar imepiga hatua kubwa katika ulinzi wa watoto baada ya kufungua mahakama mpya kwa ajili ya ulinzi wa watoto.
Mahakama hiyo ni ya tatu kufunguliwa Zanzibar na hutumika kusikiliza na kutoa hukumu za kesi kati ya familia na mtoto, mtoto mtukutu, mtoto na mtu mzima na kesi zingine za watoto wenye umri wa chini ya miaka 18.Na  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa licha ya kuwepo taasisi zinazosimamia haki na sheria lakini bado tatizo la udhalilishaji wa wanawake na watoto limeendelea kushamiri katika jamii.

Rais Shein aliyasema hayo mapema mwezi huu katika hafla ya ufunguzi wa Mahakama hiyo ya Watoto huko Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni miongoni mwa muendelezo wa sherehe za kuadhimisha Siku ya Sheria, Zanzibar kwa mwaka huu.Katika hotuba yake kwa wananchi,anasema kuwa vitendo vya aina hiyo ni kinyume na mafundisho ya dini, malezi pamoja na Katiba na Sheria zilizopo ambazo baadhi yake zimepata tunzo kwa ubora wake ikiwemo Sheria ya Mtoto Namba 6 ya mwaka 2011 ambayo imepata tunzo huko Geneva kutokana na ubora wake duniani.
Hivyo,anazitaka taasisi zinazosimamia haki na Sheria kuitumikia Serikali yao kwa uwazi na ukweli kwa lengo la kufikia malengo yaliowekwa pamoja na kuitaka jamii kutoa ushirikiano katika kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo.Aidha anasema Jamii ina dhamana kubwa ya kulea vyema watoto kwani ni dhahiri kwamba kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha haki za watoto zinalindwa na maslahi yao yanazingatiwa kuanzia kwenye ngazi za familia na siyo kwenye vyombo vya sheria pekee yake.


Halikadhalika anasema kuwa taarifa za Kitengo cha kurekebisha makosa ya urajisi cha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, zinathibitisha kuongezeka kwa kesi za aina mbali mbali katika jamii zinazovunja haki za watoto ambazo zimeripotiwa katika mwaka 2016 ikilinganishwa na mwaka 2015.Ripoti ya mwaka 2016, idadi ya kesi za watoto waliopewa ujauzito zilizoripotiwa ni 26, ikilinganishwa na kesi 19 zilizoripotiwa mwaka 2015 ambapo wamo watoto wa darasa la sita hadi Kidato cha Nne.Akiendelea na hotuba hiyo pia anasema kuwepo kwa chombo kinacho onesha vimelea vya urithi vya wazee (DNA) kamwe sio sababu ya kumaliza tatizo hilo katika jamii kwani chombo hicho kinasimamiwa na mwananadamu ambapo jambo kubwa linalotakiwa ni kubadilika na kutofanya kazi kwa mazoea.Anaeleza kuwa fedha nyingi zimetumika katika ujenzi wa jengo hilo ikiwa ni kwa lengo la kutekeleza haki za watoto sambamba na kupiga vita udhalilishaji wa watoto kwa kuuondoa kabisa kadhia hiyo huku na hivyo taasisi husika zitawekwa pamoja katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo kama alivyofanya kwenye changamoto ya takwimu hivi karibuni.


Alisema kuwa juhudi mbali mbali zimechukuliwa na Serikali katika kuhakikisha vitendo hivyo vinaondoshwa kabisa ikiwa ni pamoja kuanzisha Kampeni ya miaka miwili ya Kupiga Vita Ukatili na Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto Zanzibar iliyozinduliwa Disemba mwaka 2014  ambapo Serikali kupitia Wizara husika imeamua kufanya tathmini.Kutokana na maelezo yake Rais Shein anatoa wito kwa wananchi kujitokeza kwenda kutoa ushahidi pale unapohitajika ili kuepuka kesi za udhalilishaji kuishia majumbani hatua ambayo pia, itaisaidia Serikali kufikia malengo yake iliyojiwekea.Anatumia fursa hiyo  pia kutoa pongezi kwa Majaji, Mahakimu, Makadhi na Watumishi wote wa Mahakama kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kutoa haki kwa wananchi.

 

Akitoa taarifa ya mradi wa jengo hilo la Mahakama ya Watoto,  Mwakilishi wa Mahakama Kuu, George Joseph Kazi alisema kuwa ujenzi wa Mahakama hiyo umedhaminiwa na Shirika la Maendeleo ya Watoto Ulimwenguni (UNICEF) ambalo lengo lao kuu ni kutoa msaada wa kitaalamu na kifedha kwa ajili ya maendeleo ya haki ya mtoto kulingana na sheria ya Mtoto No. 6 ya mwaka 2011.Anasema kuwa ujenzi huo ulianza rasmi tarehe 04.10.2015 na kukamilika mwezi Desemba mwaka 2016 mradi ambao ni wa jengo moja ambalo linajumuisha Ofisi ya Hakimu wa Mahakama ya Watoto, Ofisi ya Waendesha Mashtaka, Ofisi ya Makarani, Ofisi ya Ofisa wa Ustawi wa jamii, chumba cha Computa, mapokezi na nyenginezo.


Kwa maelezo ya Mwakilishi huyo wa Mahakama Kuu, ujenzi wa Mahakama hiyo umegharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania milioni 106,996,220.Naye Mwakilishi wa UNICEF katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi Maniza Zaman katika hotuba yake alisisitiza kuwa Shirika hilo la Umoja wa Mataifa litaendelea kushirikiana na kuunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha watoto wanaendelea kupata haki zao za msingi.  
Viongozi mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamdani Omar Makame,  Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Majaji, Mahakimu na viongozi wengine wa Serikali na vyama vya siasa.

 

Sr Angela Rwezaula 

Idhaa ya Kiswahili ya Radio vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.