2017-02-15 15:40:00

IFAD epukeni miradi yenye kinzani kati ya watu mahalia na Serikali!


Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo wa Umoja wa Mataifa mwaka 2017 unaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwake. Kama sehemu ya kumbu kumbu hii, wajumbe wa Baraza kuu la IFAD kwa kushirikiana na wajumbe waliokuwa wanahudhuria Jukwaa la Tatu ya Watu Mahalia mjini Roma, wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, Jumatano, tarehe 15 Februari 2017 kwenye Ukumbi mdogo wa Paulo VI kabla ya Katekesi yake.

Mkutano huu wa IFAD anasema Baba Mtakatifu Francisko, umekuwa ni fursa ya kuibua mbinu mkakati ya kuwawezesha watu mahalia katika masuala ya kiuchumi. Changamoto kubwa ni kuweka uwiano mzuri kati ya maendeleo ya kweli na endelevu kwa binadamu, pamoja na masuala ya kijamii na kitamaduni kwa watu mahalia kadiri ya mazingira yao. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwa makini na sera pamoja na mikakati ya kiuchumi inayoweza kuingilia kati tamaduni za watu mahalia na matumizi yao kuhusu ardhi.

Hapa anasema Baba Mtakatifu, kuna haja ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za watu mahalia, ili kujenga mchakato wa ushirikiano wa amani kati ya Serikali na watu mahalia, ili kuepukana na kinzani pamoja na migogoro isiyokuwa na tija kwa ustawi na maendeleo ya watu husika. Sehemu ya pili anaendelea kusema Baba Mtakatifu ni kubainisha kanuni, miongozo na miradi itakayokuwa na utambulisho wa watu mahalia, hasa kwa kuzingatia mahitaji ya vijana wa kizazi kipya pamoja na wanawake.

Ni vyema ikiwa kama viongozi wa Serikali watatambua kwamba watu mahalia wanapaswa kushirikishwa, ili hatimaye, kuwawezesha kuchangia na kushiriki kikamilifu katika miradi iliyoibuliwa katika ngazi ya watu mahalia na hatimaye, katika ngazi ya kitaifa. IFAD inaweza kutoa mchango mkubwa katika kubainisha mwongozo huu kwa kugharimia na kutafuta wataalam waliobobea katika masuala haya, ili kuleta maboresho makubwa katika maisha ya watu, vinginevyo, anasema Baba Mtakatifu, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yasiyosaidia mchakato wa maboresho ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa watu wengi kuwa na maisha bora zaidi, hayafai hata kidogo. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru wajumbe hawa kwa kumtembelea mjini Vatican na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.