2017-02-14 15:02:00

Wahubiri zingatieni: ujasiri, sala na unyenyekevu!


Ujasiri, maisha ya sala na unyenyekevu ni mambo msingi yaliyowapambanua Watakatifu Cyril na Method, wasimamizi wa Bara la Ulaya katika maisha na utume wao; watakatifu wanaokumbukwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Februari. Hawa ni watakatifu waliochangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa umissionari, uinjilishaji na utamadunisho kiasi cha kuliwezesha Neno la Mungu kuota mizizi katika maisha na tamaduni za watu.

Hawa ni Wamissionari waliopandikiza mbegu ya Neno la Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko, kama ilivyokuwa kwa wale wafuasi Sabini na wawili waliotumwa na Yesu wawili wawili kumtangulia mahali alipokusudia kwenda. Neno la Mungu linahitaji kutangazwa na kushuhudiwa kwa ujasiri, ili hatimaye liweze kupenya katika maisha ya watu; jambo linalohitaji ukweli, nguvu na ujasiri! Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 14 Februari 2017. Baba Mtakatifu anasema, mhubiri wa Neno la Mungu hana budi kuwa na ujasiri wa maisha ya kiroho; mtu aliyejishikamana na Kristo Yesu katika upendo, kwani Kristo mwenyewe ndiye chemchemi inayomwezesha mhubiri kutenda kwa ujasiri. Kwa njia hii, Neno la Mungu linakuwa na nguvu ya kuwaunda na kuwategemeza watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anaendelea kukaza akisema, Neno la Mungu lina utajiri mkubwa wa maisha ya sala; changamoto kwa waamini kutambua kwamba, mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache, kumbe, wanapaswa kumwomba Bwana wa mavuno ili aweze kupeleka watenda kazi katika shamba lake. Hapa ujasiri wa kimissionari unasimikwa katika fumbo la maisha ya sala. Neno la Mungu linapaswa kutangazwa na kushuhudiwa katika maisha ya sala, kwani kwa njia hii, Kristo Yesu anamtegemeza mhubiri katika kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu; kwa kumwagilia mbegu ya Neno la Mungu ili liweze kukua na kuzaa mazao yanayokusudiwa, yaani utakatifu wa maisha.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Yesu anawatuma wafuasi wake kama kondoo kati ya mbwamwitu, lakini wafuasi wa Kristo wanapaswa kuwa wajasiri wa kutambua hatari iliyoko mbele yao, tayari kupambana nayo kimasomaso, kwa kutambua kwamba, nyuma yao yuko Yesu anayewasimamia na kuwainua, ili waweze kutenda kazi ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ujasiri mkuu. Lakini, dhamana hii inapaswa kutekelezwa kwa njia ya unyenyekevu, ili kugusa undani wa maisha ya watu, ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu. Umissionari wa Kanisa unafumbatwa katika maisha ya sala, ujasiri na unyenyekevu kama walivyoshuhudia Watakatifu Cyril na Methodi. Waamini wawe na ujasiri wa kuwaomba watakatifu hawa ili wawezeshe kuwa na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu kama walivyofanya wao katika maisha na utume wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.